Na Mwandishi Wetu

 

WANAFUNZI waanzilishi wa shule ya Sekondari Baobab iliyopo Mapinga Bagamoyo, Mkoa wa Pwani wameshangazwa na maendeleo ya miundombinu ya kisasa iliyojengwa katika shule hiyo.

 Waliyasema hayo siku ya tarehe 25/06/2022 walipotembelea shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2005 kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha tano na wao kuwa wanafunzi wa kwanza kabisa wa shule hiyo.

 Mmoja wa wanafunzi hao wa mwanzo kabisa wa shule hiyo, Irene Kamugisha, alisema wameshangazwa na mazingira mazuri ya shule pamoja na miundombinu  waliyoikuta tangu walipohitimu masomo miaka 14 iliyopita.

 Alisema, wao walianza masomo wakati shule haikuwa na miundombinu bora ikilinganishwa na ilivyo sasa.

 “Kwa kweli tulipofika hapa tumeduwaa sana kwa sababu haya majengo hayakuwepo wakati sisi tunasoma.   Nawashukuru walimu na uongozi wa shule kwa kunipa elimu nzuri iliyoniwezesha kujiendeleza hadi kuwa mhasibu.  Sasa hivi nafundisha masuala ya usimamizi wa fedha kwa watu na makampuni mbalimbali,” alisema

 Mwanafunzi mwanzilishi mwingine aitwaye Lucyana Muro, alisema ameshangazwa na namna Uongozi wa shule hiyo ulivyopiga hatua na kufanikiwa kujipanua kwa kujenga majengo mengi ikiwemo Zahanati ya shule, Maktaba ya Kisasa, Maabara, jengo jipya la Utawala, kuanzisha Mkondo wa wavulana na shule ya Awali na Msingi Baobab.

 Wanafunzi hao waanzilishi wameishukuru Shule kwa kuwalea vizuri kimaadili na kuwapatia elimu bora iliyowasaidia kuendelea vema na masomo ya elimu ya juu na hatimaye kuwa wataalamu katika nyanja mbalimbali kama vile Uhasibu, Uchumi, Biashara, Udaktari, nishati na gesi. Aidha, wanafunzi hao walipeleka salamu kwa Uongozi wa shule kutoka kwa mwanafunzi mwanzilishi mwenzao aitwaye Kissa G. Kasongwa ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe, kwamba  ameshindwa kufika kutokana na mwingiliano wa ratiba.

 Meneja wa shule hiyo, Sophia Mawenya alisema Shule ilianza ikiwa na wanafunzi 25 tu wa Kidato cha kwanza lakini kadri muda ulivyokwenda kasi ya wanafunzi ilizidi kuongezeka kutokana na ufaulu wa wanafunzi kuwa mzuri hata kuweza kutoa wanafunzi bora kitaifa (Tanzania One) kwenye  Mitihani ya Taifa ya Kidato cha 4 na cha 6.

Alisema Dk. Jakaya M. Kikwete ndiye aliyeizindua rasmi shule hiyo mwaka 2007 akiwa Rais wa awamu ya nne na baada ya hapo idadi ya wanafunzi ilizidi kuongezeka.

 Aidha, aliwaasa wanafunzi wa shule hiyo kuwa iwapo wanataka mafanikio kwenye maisha yao basi hawana budi kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu nzuri  kwani hakuna mafanikio yanayoweza kuja bila mhusika kujituma na kuwa na nia thabiti ya kufanikiwa.  

 Aliwaeleza wanafunzi wanaosoma sasa shuleni hapo kuwa wanapaswa kujifunza kutoka kwa wenzao waliosoma hapo na kupata mafanikio.

 Aliendelea kueleza kuwa wanafunzi hao waanzilishi wana maisha mazuri kwa sababu walikuwa wanajituma katika kusoma na kuwa na  nidhamu nzuri.

Aliwaasa kuacha kuiga mambo wanayoyaona kwenye mitandao na Runinga.

Wanafunzi waanzilishi wa shule ya sekondari Baobab walioketi wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa serikali za wanafunzi (mkondo wa wasichana na wavulana) walipotembelea shule hiyo hivi karibuni
Meneja wa shule ya Baobab, Sophia Mawenya akizungumza kwenye hafla ya kuwakaribisha wanafunzi waanzilishi wa shule hiyo walipoitembelea hivi karibuni kuangalia maendeleo yake
Lucyana Muro ambaye ni miongoni mwa wanafunzi waanzilishi wa shule ya Sekondari, Baobab ya Mapinga Bagamoyo, akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo alipotembelea yeye na wenzake shuleni hapo mwishoni mwa wiki kuangalia maendeleo ya shule hiyo 




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...