NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chamwino, Deo Ndejembi amesema kwamba Jimbo hilo linatarajia kupata neema ya kujengwa kwa Hospitali kubwa mahususi kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa Fistula sambamba na kutoa huduma zingine za magonjwa ya uzazi ambayo itagharimu takribani Sh Bilioni 2.

Ndejembi ametoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara ya kuzungumza na wananchi wa Jimbo hilo la Chamwino Mkoani Dodoma katika Kata za Manchali na Majereko.

Akizungumza na Wananchi wa Kata hizo, Ndejembi amesema ujenzi huo utasimamiwa na Taasisi ya Maternity Afrika ikiwa ni jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kuwaletea maendeleo Watanzania.

" Kazi kubwa inayofanywa na Rais wetu Samia ya kuimarisha mahusiano na Mataifa mengine na Taasisi mbalimbali imekua na neema kwetu wananchi wa Kata ya Manchali na Jimbo letu la Chamwino ambapo sasa kupitia Taasisi ya Maternity Afrika tunakwenda kupata Hospitali kubwa ya kisasa ambayo itakua inafanya upasuaji mkubwa wa ugonjwa wa Fistula sambamba na magonjwa mengine ya uzazi.

Tunampongeza Rais kwa sababu kupitia mahusiano mazuri ambayo anayatengeneza na Taasisi na Mashirika binafsi Jimbo letu la Chamwino na Mkoa wa Dodoma tunakwenda kupata neema hii ya kuwa kituo cha kutibu magonjwa haya.

Tayari Taasisi hii imeshapata kibali kupitia Ofisi ya Rais Tamisemi na muda wowote kuanzia sasa ujenzi wa Hospitali hii utakwenda kuanza, niwaombe wananchi wenzangu kuendelea kuunga mkono jitihada hizi zinazofanywa na Serikali yetu kwa sababu lengo haswa ni sisi wananchi kupata maendeleo," Amesema Ndejembi.

Amesema ujenzi wa Zahanati ya Kata ya Manchali tayari umeshakamilika na kwamba ndani ya muda wa wiki moja Zahanati hiyo itazinduliwa ili ianze kutoa huduma kwa wananchi wa Kata hiyo na maeneo jirani.

" Niwape habari njema kwamba Zahanati yetu ya Manchali tayari imeshakamilika na tunatarajia baada ya wiki kutokea sasa itaanza kufanya kazi ya kutoa huduma, hii ilikua ahadi yangu wakati naomba kura mwaka 2020 na sasa nina furaha kuwaambia kwamba tumekamilisha," Amesema Ndejembi.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...