Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MKUU wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dk.Joyce Nyoni amewashauri wazazi na walezi kuhakikisha wanatenga muda wa kutosha kuzungumza na watoto wao kujadili masuala mbalimbali ili kuwaepusha watoto wasiingie katika changamoto zikiwemo za ukatili wa kijinsia.

Ameyasema hayo leo akiwa katika Banda la Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum alipokuwa katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea Viwanja vya Sabasaba mkoani Dar es Salaam.

Dk.Nyoni amesema wapo katika maonesho hayo kuelezea majukumu ambayo yanafanywa na Taasisi ya Ustawi wa Jamii kupitia  Kituo cha Elimu , Ushauri na Msaada wa Kisaikolojia.

Amefafanua kutokana na changamoto zilizopo katika jamii kumekuwa na matukio mengi ya ukatili wa kijinsia, migororo katika familia na hata sehemu za kazi, hivyo wao moja ya kazi yao ni kutoa elimu, kushauri na kutoa msaada wa kisaikolojia.

Pamoja na hayo amesema wazazi wanapaswa kuzungumza na watoto wao na kujenga urafiki ambao utasaidia katika kujadiliana mambo mbalimbali na hivyo kusaidia kuepusha changamoto nyingi ambazo huenda zingetokea kwa kukosa ukaribu kati ya mtoto na mzazi.

“Mtoto akiwa mdogo kabisa unaweza kumwambia hakikisha wewe mtu hagusi hapa na hapa ila ni mama tu anaruhusiwa, kwa hiyo ni maneno rahisi tu lakini kadiri anavyokuwa unaendelea kukua unawambia.

“Sisi kama wazazi tunatakiwa kufikisha taarifa sahihi kwa watoto wetu ila kwa bahati mbaya tumeacha wanatafuta taarifa sehemu nyingine,”amesema Dk.Nyoni na kuongeza kama mzazi atakuwa na mahusiano ya karibu na mtoto hata akikutana na mtu ambaye sio mwema atarudi kwa mzazi na kumueleza.

“Wazazi tupate muda wa kukaa na watoto, tunatafuta fedha ndio lakini mwisho wa siku ili iwe nini?Upeleke mtoto wako kliniki kwasababu ya uraibu ameharibikiwa na maisha, hapana,tunatafuta fedha sawa lakini isitangulie familia.Watoto iwe kwanza ili anapokutana na changamoto aje akwambie,”amesema.

Aidha Dk.Nyoni amesema kupitia Kituo cha Elimu ,Ushauri na Msaada wa kisaikolojia wamekuwa wakienda kuzungumza na wanafunzi katika shule za msingi na sekondari na kuwapa elimu ambazo zitawasaidia katika kukua kwao lakini wanafanya kazi na jamii.

Akizungumzia Kituo cha Elimu, Ushauri na Msaada wa Kisaiokolojia, amesema kituo hicho kipo chini ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii iliyopo katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

“Ni kituo ambacho kinatoa ushauri kama kilivyo jina lake, kinatoa elimu, kinatoa ushauri na kinatoa msaada wa kisaikolojia, tunaposema elimu maana yake tunatoa elimu ya makuzi na malezi ya watoto, elimu ya mahusiano.Tunatoa msaada kisaikolojia, maisha yanavyokwenda siku hizi tumesikia visa vya ukatili, kuna changamoto nyingi lakini inatokana na msongo wa mawazo ambao mtu anakuwa nao na kukata tama.

“Kwa hiyo na sisi tunatoa msaada wa kisaikolojia kumrudisha mtu katika ile hali ambayo anaweza kuwa na manufaa katika jamii.Kwa wale wenye changamoto ya msongo wa mawazo wanaweza kukimbilia katika kituo chetu ambacho kipo Kijitonyama katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii au wakimbilie kwa maofisa ustawi wa jamii.”

Amesema katika eneo la ukatili wa kijinsia hakuna takwimu za kisayansi ambazo zimefanyika lakini kwa kuangalia kwa haraka  tatizo ni kubwa kwani hata katika familia nyingi utabaini kuna migogoro.

Amesema changamoto wanayoiona kama Taasisi ni watu kutotambua kama kuna mahali pa kupata msaada kuhusu yale yanayowakabili, kijana anapata changamoto katika mahusiano basi anakata tamaa ya maisha, kumbe kuna mahali anaweza kwenda kupata ushauri na mambo yakawa sawa sawa.

Wiziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk.Dorothy Gwajima(wa sita kutoka kushoto) akiwa pamoja na Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dk.Joyce Nyoni(watano kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Taasisi hiyo baada ya kutembelea banda lao lilipo katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara

Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dk.Joyce Nyoni akifafanua jambo kuhusu kazi zinazofanywa na Kituo cha Elimu, Ushauri na Msaada wa Kisaikolojia ambacho kipo chini ya taasisi hiyo.

Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dk.Joyce Nyoni(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa taasisi hiyo wakiwa katika banda lao lililopo katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea Viwanja vya Sabasaba mkoani Dar es Salaam.

Mmoja ya maofisa wa Kituo cha Elimu, Ushauri na Msaada wa kisaikolojia kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii akielezea jambo kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum (katikati) baada ya kutembelea banda la Wizara hiyo.


Wiziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makudi Maalum Dk.Dorothy Gwajima akisoma moja ya chapisho ambalo limeandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii ambalo linaelezea kwa kina kuhusu taasisi hiyo pamoja na Kituo cha Elimu, Ushauri na Msaada wa kisheria.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...