Na Joseph Lyimo


WANAWAKE wa jamii ya kifugaji wa Wilaya ya Simanjiro na Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara, wengi wao wamechangamkia fursa ya kupatiwa chanjo ya maambukizi ya UVIKO-19 kutokana na kuwahofia baadhi ya wanaume zao wanaosafiri kwenda maeneo mbalimbali ili kujikimu kimaisha.

Baadhi ya wanaume wa jamii ya wafugaji waliotoka Wilaya ya Simanjiro na Kiteto, wamejitosa maeneo mbalimbali nchini ikiwemo jiji la Arusha, Dodoma, Dar es salaam na maeneo ya nchi jirani ikiwemo Kenya, Zambia, Malawi, Uganda hadi Afrika kusini.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wanawake wa jamii hiyo ya kifugaji wamechangamkia fursa ya kupata chanjo ya UVIKO-19 ili wasipate maambukizi kutokana na wanaume wao kusafiri mbali na kisha kurudi nyumbani kwao wakihofia maambukizi hayo.

Mkazi wa kijiji cha Loiborsoit A Wilayani Simanjiro, Esupati Saitoti (25), anaeleza kuwa yeye binafsi amepata chanjo ya UVIKO-19, kutokana na kuwa na hofu ya kuambukizwa na mume wake ambaye anafanya kazi ya ulinzi wa nyumba jijini Dar es salaam.

“Kutokana na kuwepo na UVIKO-19 hapa nchini tangu ilivyoingia mwaka 2020 ilinibidi nipate chanjo kwa kuhofia kupata maambukizi kwani mume wangu ni mtu wa kusafiri hivyo angeweza kuleta nyumbani pindi akifika kutoka Dar es salaam,” anasema Esupati.

Anaeleza kwamba amezaa na mume wake watoto watatu na anaishi na watoto hao huku mume wake ambaye hakutaka kumtaja jina lake anaishi jijini Dar es salaam, huku akifanya kazi ya ulinzi kwenye nyumba moja.

“Nilichanja baada ya jirani yangu mmoja kufariki yeye na mke wake kwani alikuwa anafanya kazi ya kusuka wanawake nchini Zambia na UVIKO-19 ulivyoingia nchini mwaka 2020 alirudi kutoka Zambia kumbe alikuwa nao akamuambukiza mkewe wakafa wote wawili,” anasema kwa majonzi Esupati.

Anasema awali hakutaka kuchanja kutokana na baadhi ya watu kutoa dhana potofu kuwa chanjo ya UVIKO-19 ina madhara jambo ambalo siyo sahihi kwani yeye ameshachanja na hakuathirika kama ilivyokuwa inasemwa.

“Mimi nilichanja na baada ya muda mfupi nilijisikia homa kidogo na kichefuchefu ila sikutapika japokuwa baada ya muda wa saa moja nikawa sawa tuu nikapumzika na kuendelea na shughuli zangu za kawaida za kila siku,” anasema.

Mkazi wa Kata ya Loolera Wilayani Kiteto, Salome Saruni anasema kuwa baadhi ya wanaume wa jamii ya kifugaji walivyotoka kijijini kwao na kwenda maeneo mbalimbali ya mijini na nje ya nchi kwa ajili ya ususi, kuuza dawa za asili na kulinda nyumba kumechangia wao kuitikia kuchanja.

“Wengi wa wanawake wa jamii ya kifugaji awali hatukuwa na mwamko wa kuchanga kutokana na kutumia dawa za asili pindi tukiugua ila baada ya kuona baadhi ya wanawake na wanaume wanakufa kutokana na kuletewa ugonjwa huo ikatubidi tuchanje,”

Diwani wa viti maalum Tarafa ya Emboreet Wilayani Simanjiro, Namnyaki Edward anaeleza kuwa mwitikio wa wanawake wa jamii ya wafugaji kuchanja haukuwa mkubwa awali ila baada ya kuthibitika kuwa baadhi ya wanaume wanaofanya shughuli za kiuchumi nje ya nyumbani ndiyo wanaeneza ikabidi wawe wanachanja.

“Mimi binafsi nimechanja baada ya mganga mkuu wa mkoa Dk Damas Kayera kufika Orkesumet makao makuu ya wilaya na wataalam wengine wa afya wakatupa elimu sisi madiwani wa Simanjiro, kisha tukachanja,” anasema Namnyaki.

Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto, (DAS) Fadhili Alexander anasema kwamba hivi sasa wameanza hamasa ya uchanjaji wa chanjo ya UVIKO-19 kwa wananchi wote hivyo jamii inapaswa kuchangamkia fursa hiyo.

Anaeleza kuwa wananchi wenye umri wa kuanzia miaka 18 kwenda juu wanapaswa kujitokeza kupata chanjo hiyo kwani jamii haitachangia fedha yoyote katika kupata huduma hiyo.

“Naomba wananchi wote tujitokeze kupata chanjo ikiwemo mimi na wewe kwani viongozi na jamii kwa ujumla tunapaswa kuhamasishana ili tufanikishe suala hili,” anamalizia kwa kusema DAS huyo.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...