Na Mwandishi Wetu, Sikonge

CHAMA Cha Mapunduzi (CCM) kimekemea tabia ya baadhi ya watumishi wa halmashauri nchini kukwamisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa sababu ya kutaka ‘Ten Pacent’ (rushwa) kutoka kwa wakandarasi, hali inayosababisha miradi kutokamilika au kufanyika.

Akizungumza jana na wananchi wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alisema Chama kinafuatilia kwa karibu mwenendo wa baadhi ya watumishi hao wanakwamisha miradi ya maendelo kwa kutaka rushwa kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo.

“Tumekuja kukagua uhai wa Chama chetu na utekelezaji wa Ilani, Chama chetu ndicho kimeunda Serikali, nichukue fursa hii kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi za maendeleo, anazopeleka kwenye wilaya mbalimbali ikiwemo hii ya Sikonge. Sasa fedha nyingi zilizoletwa ziendane na kasi za utekelezaji wa maendeleo endelevu ambayo Rais ameelekeza yafanyike kupitia miradi ya kimkakati.

“Bahati nzuri Rais Samia anajua na anafahamu mahitaji ya wanachi anawaongoza, kwa hiyo kila wilaya na kila Mkoa ametoa vipaumbele na kipaumbele cha kwanza ni huduma za afya kwa jamii na ndio maana hata Wilaya ya Sikonge kwenye hospitali hii ya Wilaya Rais ametoa Sh. bilioni mbili.

“Sasa ujenzi huu wa miradi hii mikubwa ya maendeleo uendane na utoaji bora wa huduma kwa wananchi, majengo haya ambayo yanajengwa , vitendea kazi ambavyo vinawekwa, kwa sababu lazima niseme jambo moja ambalo rais amelifanya anajenga majengo na wakati huo huo analeta na vifaa tiba,” alisema Shaka.
Aliongeza kuwa katika historia ya nchi hii, Rais Samia amekuwa wa kipekee kwani huko nyuma majengo yalikuwa yanajengwa baadae yanabaki kuwa mazalia ya ndege, lakini leo hii wanajenga na wanaweka vifaa vya kisasa, niwaombe wauguzi, madaktari pamoja na wote ambao mnahusika kwa njia moja ama nyingine katika kutoa huduma za afya kwa wananchi lazima wawe rafiki kwa wateja wao.

“Lazima mtengeneze mazingira bora ya kuhakikisha huduma hizi ziendane na kasi ambayo Rais wetu amekuwa akiionesha , bahati mbaya sana na kwa masikitiko makubwa na hili naomba niseme kwenye baadhi ya wilaya ikiwemo hii ya Sikonge kwenye miradi hii ya maendeleo kasi ya uendelezaji na ukamilishaji miradi sio nzuri.

“Haifurahishi kabisa kasi , fedha zinakuja kwenye halmashauri lakini kasi ya ukamilishwaji wa miradi na uanzishwaji wa miradi imekuwa ikisuasusa jambo hilo sio nzuri ,spidi ya Rais Samia kwenye miradi ya maendeleo ni kubwa mno.Sasa panapotokea sehemu pakalegalega , mambo yakawa yanaenda kama ambavyo hatukuyatarajia Chama hatuwezi kufunga funga maneno na hatuwezi kukaa kimya,”alisema Shaka.

Aliwaomba waliopewa dhamana ya katika Serikali watimize wajibu wao wa kumsaidia Rais Samia kutektekeleza yale aliyoyakusudia kwa wananchi badala ya kuwa sehemu ya wakwamishaji.

“Kwenye hili sitafungafunga maneno halmashauri ya Sikonge itabidi mjitathimini na mambo hayaendi vizuri , wako maofisa wamekuwa ni sehemu ya ukwamishaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo, haiwezekani miradi hii inakwama wakati mwingine kwasababu ya wakandarasi kuombwa rushwa iliyokithiri ili ndio wakamilishe hii miradi.

“Taarifa tunazo na tunawajua wanaofanya haya tunawajua , narejea tena taarifa tunazo baadhi ya watumishi wa halmashauri mjitathamini mnachokifanya sio sahihi.Sababu moja ya kukwama miradi hii isianze kwa wakati, sababu moja ya miradi hii kutokamilika kwa wakati baadhi ya watumishi wa halmashauri mnataka cha juu kikubwa , mnawakwamisha wakandarasi,”alisema.

Shaka alisema kwa hiyo wanaposema shughuli za maendeleo zinasuasua na haikamiliki kwa wakati kuna watu wanakwamisha, na hivyo ameomba TAKUKURU wafanye kazi yao na wakitaka CCM inaoneshe njia watawaonesha kwani wanafahamu yanayofanyika.

Aliwataka watendaji waliokabidhiwa dhamana katika halmashauri kuhakikisha wanawafikia waanchi katika maeneo wakiwemo wa vijijini ili kuwasikiliza na kutatua shida zao ambapo ametoa mfano wilayani Sikonge kuna baadhi ya maeneo wananchi wanalalamika kutofikiwa watumishi.

“Tumsaidieni Rais Samia kuwafikia wananchi kutatua kero zao na changamoto zao, ndio jukumu tulilopewa, tusipofanya hivyo itakuwa sehemu ya kukwamishana na mambo hayataenda vizuri,” alisema.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, akitazama asali iliyochakatwa katika kiwanda cha kuchakata asali wilayani Sikonge, Mkoa wa Tabora akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mkoani humo.


Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndg. Shaka Hamdu Shaka, akisikiliza maelezo kuhusu kukwama kwa Mradi wa Kiwanda cha Nyuzi Tabora

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, akitazama mitambo katika kiwanda cha kuchakata asali wilayani Sikonge, Mkoa wa Tabora akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mkoani humo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...