Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC,) Nehemia Mchechu akizungumza na Chama cha Wafanyabiashara Afrika Kusini katika kikao kilichowakutanisha kwa lengo la kujadili fursa za uwekezaji katika sekta ya nyumba, Mchechu amesema NHC itaendelea kulitangaza shirika hilo ili kuvutia wawekezaji wakubwa na wadogo kutoka ndani na nje ya nchi.
 

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC,) limekutana na Chama cha Wafanyabiashara cha Afrika Kusini na kwa lengo la kuwaeleza nini NHC inafanya na fursa lukuki za uwezekaji zinazopatika kupitia shirika la  nyumba nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC,)  Nehemia Mchechu amesema, NHC inaamini katika uwekezaji wa ndani na nje na uchumi mzuri wa Afrika Kusini unahitaji uwekezaji mkubwa ikiwemo katika sekta ya nyumba kwa nchi kama Tanzania ili azma ya kuwa na makazi bora kwa wananchi ifanikiwe kwa kiwango kikubwa zaidi sambamba na kutengeneza ajira  kwa watanzania.

 Mchechu amesema, kupitia kampeni ya 'Royal Tour' iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan NHC itaendelea kutembea nayo na kulitangaza shirika hilo ili kuvutia wawekezaji wakubwa na wadogo kutoka ndani na nje ya nchi.

''Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akielekeza na kusisitiza umuhimu wa sekta binafsi katika kuchangia maendeleo ya Nchi…Sekta binafsi ndiyo itafanya biashara na serikali itabakia kusimamia sera za kuwajengea mazingira rafiki wawekezaji ikizingatiwa kuwa, hapa nchini kuna fursa muhimu za kibiashara ikiwemo uongozi imara.’’ Amesema Mchechu.

 Akieleza mipango ya NHC Mchechu amesema kwa mwaka huu wa fedha shirika hilo litatumia  Bilioni 413.7 kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa nyumba kwa wananchi wa hali ya chini na kati ambapo nyumba 5000 zitajengwa kupitia mpango  wa Samia Housing Scheme (SHS.)

''Mradi huu wa nyumba za kuuza na kupangisha nyumba wa SHS, umelenga  kuenzi kazi nzuri anazofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kuletea maendeleo na tunatamani watanzania  wamkumbuke kwa jitihada hizo baadaye.’’ Amesema.

Amesema kuwa asilimia 50 ya nyumba hizo zitajengwa jijini Dar es Salaam,  asilimia 20 Dodoma na mikoa mingine ya Tanzania asilimia 30 na kwa Mkoa wa Dar es Salaam ujenzi wa nyumba 500 zitajengwa kuanzia mwezi Septemba mwaka huu  katika eneo la Kawe na Medeli jijini Dodoma nyumba 100 zitajengwa.

 Mchechu pia ameushukuru   Ubalozi wa Afrika Kusini Nchini Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na  kuwashirikisha fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania wawekezaji kutoka Afrika Kusini.

Akieleza mikakati ya NHC Mchechu amesema, Shirika linapanga utekelezaji wa miradi mipya ya sekta ya nyumba pamoja na mpango wa kushirikiana na sekta binafsi utakaozinduliwa mwezi huu pamoja na kutekeleza miradi mipya ya makazi katika jiji la Dar es Salaam itakayowanufaisha wananchi wa hali zote pamoja na kumalizia miradi ya kimkakati iliyokwama kutokana na sababu mbalimbali.

 Pia amesema, miradi ya ujenzi wa nyumba katikati ya jiji la Dar es Salaam ikiwemo Kawe, Kinondoni, Mchikichini, Temeke utatekelezwa na shirika hilo kwa kushirikiana na sekta binafsi na ujenzi huo utajibu changamoto za makazi, biashara na watanzania wataishi  na kuweza kununua nyumba hizo kwa gharama nafuu, na watakaopewa kipaumbele katika makazi hayo ni wakazi waliokuwa wakiishi hapo na wananchi wengine wenye uhitaji.

Aidha amesema kuwa NHC mejipanga katika kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya nyumba na watakutana na   waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali nchini wakiwa kiungo muhimu na kueleza mikakati ya sekta ya nyumba.

 Mkurugenzi wa Chama cha Wafanyabiashara wa Afrika Kusini wanaofanya biashara na kuwekeza nchini Manish Thakra akizungumza katika kikao hicho.

Vilevile Mkurugenzi wa Chama cha Wafanyabiashara wa Afrika Kusini wanaofanya biashara na kuwekeza nchini Manish Thakrar amesema, NHC imetangaza fursa nyingi ambazo wameona ni vyema washiriki fursa hiyo ya uwekezaji hasa katika miradi ya sekta ya nyumba za makazi.

Ameeleza NHC imeonesha miradi ambayo nchi yoyote duniani inaweza kuwekeza na ushirikishwaji wa sekta binafsi unaofanywa na NHC utaleta matokeo chanya katika kutatua changamoto ya makazi kwa wananchi hasa katika maeneo ya miji na kuzitaka nchi za Afrika kuiga mfano huo kwa utekelezaji na kuja kuwekeza katika ardhi ya Tanzania ambayo mazingira yake yana tija kwa manufaa ya biashara na jamii.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...