Na Mwandishi wetu, Simanjiro

HALMASHAURI ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara imepongezwa kwa kushika nafasi ya pili kitaifa kwenye kukusanya mapato kati ya Halmashauri 185 zilizopo nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera ametoa pongezi hizo wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro cha kusoma taarifa za kata 18.

Dk Serera amesema Simanjiro imeshika nafasi ya pili kwa kushinda vigezo saba ambavyo ni ukusanyaji wa mapato na kupeleka fedha kwenye miradi mingi ya maendeleo.

Amesema vigezo vingine walivyoshinda ni kutoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na wenye ulemavu na kufuatilia marejesho ya mikopo.

“Pia Simanjiro imeonekana bora kwenye matumizi ya fedha za marejesho ya kukopesha vikundi vingine, kujibu hoja za CAG na mawasiliano na umma kuhusu shughuli za serikali,” amesema Dk Serera.

Amewataka wawe wabunifu kwa kuhakikisha wanabuni vyanzo vingine vya mapato ili nyakati nyingine washike nafasi ya kwanza kwani uwezo huo wa kuongoza Simanjiro wanayo.

“Sisi tuliozoea kushika nafasi ya kwanza huwa tunahitaji kuwa kwenye nafasi hiyo hiyo, hivyo ongezeni mshikamano na ushirikiano katika makusanyo yenu,” amesema Dk Serera.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Samwel Warioba amewapongeza wale wote waliofanikisha wao kushika nafasi ya pili kitaifa kwa makusanyo.

“Tumekwama kidogo tuu kupata nafasi ya kwanza, ila hatujachelewa tujitahidi kuhakikisha wakati ujao tunafanya vyema zaidi ya hapa tulipofika,” amesema Warioba.

Amesema sivyo vyema Halmashauri hiyo kushika nafasi ya pili kisha wakati ujao wakashuka chini, kwani macho ya wengi yapo Simanjiro wakisubiri kipindi kijacho kupaa zaidi.

Diwani wa Kata ya Loiborsoit, Baraka Kiduya amepongeza hatua hiyo kwani imepandisha morali kwa wananchi wa Wilaya ya Simanjiro katika kuiunga mkono Halmashauri yao.

“Nawapongeza Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi mtendaji, watumishi, madiwani na wananchi kwa ujumla kwa kufanikisha ushindi huo wa pili,” amesema Kiduya.

Tanzania ina jumla ya halmashauri 185 na Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro ndiyo imekuwa ya pili kwa kupata alama 88.7 kati ya 100 huku ikifikisha asilimia 140 ya ukusanyaji wa mapato.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...