Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi tuzo Bi. Rukia Mtingwa Meneja Uhusiano wa kampuni ya MIC Tanzania wamiliki wa Makampuni ya simu ya Tigo na Zantel kutokana na mchango wao kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, wakati alipohudhuria mkutano maalum wa wadau wa Sekta Binafsi, 15 Agosti, 2022 Katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Mhe. George Simbachawene wakati alipohudhuria mkutano wa wadau wa Sekta binafsi juu ya ushiriki wao katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, 15 Agosti 2022 Katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala na kulia ni Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara Anne Makinda.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wadau wa Sekta binafsi juu ya ushiriki wao katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, 15 Agosti, 2022, Dar es Salaam. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi tuzo Mkurugenzi wa Benki ya Stanbic Bw. Kevin Wingfiel  kutokana na mchango wao kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, wakati alipohudhuria mkutano maalum  wa wadau wa Sekta Binafsi, 15 Agosti, 2022 Katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi tuzo Bi. Annette Kanora ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom kutokana na mchango wao kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, wakati alipohudhuria mkutano maalum wa wadau wa Sekta Binafsi, 15 Agosti, 2022 Katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi zitawasaidia wafanyabiashara kutathmini uwezo wao wa kibiashara au uwezo wa mitaji kutoa faida na kutafuta maeneo mapya ya uwekezaji.

 

Wafanyabishara wakubwa kwa wadogo hutumia takwimu za sensa kutathmini uwezo wa kibiashara wa makampuni, uwezo wa mitaji kutoa faida na kutafuta maeneo mapya ya uwekezaji na kupitia takwimu za sensa, menejimenti na bodi za makampuni ya biashara na taasisi za uwekezaji za ndani na nje hupata uhakika wa kitakwimu ambao huwaongezea kujiamini na kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati,” amesema.

 

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Agosti 15, 2022) wakati akizungumza na wadau wa sekta binafsi juu ya umuhimu wa ushiriki wao kwenye Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika nchini Agosti 23, 2022 kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

 

Amesema wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo wanategemea takwimu za sensa kufanya maamuzi ya uwekezaji ikiwemo huduma mbalimbali kama maduka makubwa, upanuzi wa shughuli zao kama maghala ya kuhifadhia na kusambazia bidhaa, maeneo bora ya kutangaza biashara zao, masoko mapya na kubuni bidhaa mpya pamoja na aina ya huduma kama za hospitali, sehemu za starehe na sehemu za kufanyia mazoezi.

 

Amemshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia, kuthamini na kutilia mkazo mkubwa masuala ya takwimu na kuruhusu mwaka huu Tanzania ifanye Sensa kwa mujibu wa Miongozo ya Umoja wa Mataifa.

 

“Kitendo cha Mheshimiwa Rais kuridhia kutekeleza sensa ya sita mwaka huu kinaonesha uimara wa  uongozi wa Kiongozi wetu na utekelezaji wa takwa hili ni kwa faida ya nchi yetu na ulimwengu kwa jumla.”

 

“Sensa ya Watu na Makazi ni muhimu kwa kuwa moja ya mikakati ya kiuchumi ya Tanzania ni kuvutia uwekezaji na kuboresha kiwango cha maisha cha wananchi wake. Uwepo wa takwimu bora za Sensa ya Watu na Makazi utasaidia kuharakisha utekelezaji wa mikakati hiyo,” amesema Waziri Mkuu.

 

Akizungumzia umuhimu wa sensa kwa wafanyabiashara Waziri Mkuu amesema: “Kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara, sensa ni chanzo cha msingi cha taarifa za kidemografia na ukuaji wa soko la bidhaa na huduma katika nchi zote duniani. Takwimu zote za biashara zinahitaji takwimu za idadi ya watu kama kigezo cha msingi cha kufanya maamuzi ya uwekezaji, uzalishaji na biashara.”

 

Ametoa pongezi pia kwa vyombo vya habari kwa ushiriki wao mkubwa katika kutoa hamasa kwa jamii na kuwaelezea umuhimu wa sensa ikiwemo kuwajulisha kuwa sensa hiyo itafanyika lini. Amesema utafiti uliofanywa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) Julai mwaka huu ulionesha kuwa asilimia 98 ya Watanzania wanatambua uwepo wa sensa

 

“Kitendo cha kuwaonesha wananchi nini kitaulizwa, kimesaidia kuwaandaa wananchi kuhusu zoezi hili. Wasanii mbalimbali nchini wametoa elimu kwa kiwango kikubwa, viongozi wa dini nao wamefanya kazi kubwa na nzuri sana ya kuwaandaa wananchi, ninawashukuru sana.”

 

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wadau hao, Waziri wa Nchi (OWM-SBU), Bw. George Simbachawene alisema mpaka sasa maandalizi ya zoezi la sensa yamefikia asilimia 95. “Asilimia hii tano iliyobakia tusiidharau. Kulingana na muda uliobaki, mimi pamoja na wenzangu tutajitahidi ili tufike kwenye ufanisi unaotarajiwa wa asilimia 100,” alisema.

 

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Bw. Paul Makanza alisema wameshirikiana na Serikali katika vikao kadhaa na kuainisha maeneo saba ambayo wanaweza kuunga mkono.

 

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni utoaji wa huduma, vifaa, utoaji elimu, usafiri, usafirishaji wa vifaa, utoaji wa matangazo na kuchangia mafuta ya magari. Alisema baadhi ya kampuni za simu zilianza kurusha jumbe fupifupi kwa wateja wao, vituo vya redio na televisheni navyo vilianza matangazo kuhamasisha jamii.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...