Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji zimeahidi kuongeza ushirikiano ili kuongeza ufanisi katika shughuli za bandari pamoja na Chuo cha Bandari nchini.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kijavara amebainisha hayo wakati alipokutana kwa mazungumzo na Uongozi wa Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bandari hiyo Bw. Kristof Waterschoot katika Ofisi za Mamlaka hiyo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia ugeni huo, Mhandisi Kijavara amesema umetembelea bandari hiyo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina yao na kuona maeneo gani wanaweza kuanzisha ushirikiano na kukuza ufanisi wa huduma za bandari.
“Tumeona tushirikiane na wenzetu walioendelea zaidi katika bandari ili kuboresha ufanisi katika bandari zetu na maeneo tunayoona ni ya kipaumbele ni ushirikiano katika kuboresha Chuo chetu cha bandari, kuimarisha shughuli za bandari za kila siku, miundimbinu na masuala ya Tehama,”amesema Kijavara.
Pamoja na mambo mengine, Kijavara amesema kwa mwaka wa kalenda 2021 walihudumia meli 50 - 60 kwa mwezi lakini kutokana na kuongezeka kwa ufanisi, TPA inahudumia meli kati ya 65 - 80 kwa mwezi na kuchangia makusanyo kuongezeka kutoka Sh bilioni 70 - 75 kwa mwezi hadi kufikia Sh bilioni 90 - 100 kwa mwezi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji, Bw. Kristof Waterschoot amesema kuwa lengo la ziara yake nchini ni kuangalia maeneo ya ushirikiano baina ya Bandari ya Antwerp na Mamlaka ya Bandari ya Tanzania ili kuboresha zaidi ufanisi wa bandari pamoja na Chuo cha Bandari ili kuweza kuwajengea uwezo zaidi wanafunzi wanaosoma na watakaosoma katika chou cha bandari.
“Tunaamini ushirikiano baina ya Bandari ya Antwerp na TPA utaimarisha sekta ya bandari zetu na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za bandari kwa maslahi ya mataifa yetu,” amesema Bw. Waterschoot    
Uongozi wa Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji umewasili nchini leo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo mbali na kuitembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), pia ujumbe huo utafanya ziara katika Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) pamoja na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Jijini Dodoma.
Balozi wa Ubelgiji nchini, Mhe. Peter Huyghebaert akifuatilia kikao baina ya Ujumbe wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji, Bw. Kristof Waterschoot kilichofanyika katika ofisi za Bandari Jijini Dar es Salaam.
Kikao kikiendelea baina ya Ujumbe wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na ujumbe wa Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji kikiendelea katika ofisi za Bandari Jijini Dar es Salaam.Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji, Bw. Kristof Waterschoot akieleza jambo wakati wa kikao kati yake na Ujumbe wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA). kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za Bandari Jijini Dar es Salaam.Ujumbe wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na katika pichaa ya pamoja na Ujumbe wa Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji.
Ujumbe wa Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji ukipata ufafanuzi wa shughuli mbalimbali za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ulipofanya ziara katika bandari hiyo leo Jijini Dar es Salaam

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...