Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imejipanga kuanzisha mpango wa wananchi wote kufanya mazoezi ya kutembea na kukimbia ikiwa na kauli mbiu ya “fanya mazoezi na JKCI kwa siku tatu za wiki linda moyo wako” ili kupunguza magonjwa ya moyo ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi katika jamii.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya ofisi leo Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kwa kushirikiana na wizara ya afya atahakikisha suala la mazoezi linapewa kipaumbele ili kujenga jamii yenye afya bora.

Dkt.Kisenge alisema ataiomba Wizara ya afya kwa pamoja wawe na slogani ya kufanya mazoezi ya matembezi nchi nzima ambapo wananchi ambao watatembea kilometa ambazo watakuwa wamezipanga watapewa unafuu wa kufika JKCI kupatiwa matibabu ya moyo bila malipo ikiwa ni njia ya kuwahamasisha wananchi kufanya mazoezi.

Akizungumzia uteuzi wa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Kisenge aliahidi kudumisha utendaji mzuri uliofanywa na Prof. Mohamed Janabi tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo miaka saba iliyopita kwa kuifanya Taasisi hiyo kukuwa kwa kasi na kujulikana hapa Tanzania na nje ya nchi.

Dkt. Kisenge alisema JKCI itaendelea kuboresha huduma za matibabu ya moyo hapa nchini kwa kuwawezeshea wananchi kupata huduma bora zaidi na kuwafuata mahali walipo ili kuwapatia matibabu lakini pia kuwafundisha madaktari waliopo mikoani ili waweze kujua jinsi gani wanaweza kuwasaidia wagonjwa wa moyo.

“Tutaongeza vifaa tiba na miundombinu ambayo itawasaidia madaktari wetu kuweza kufanya upasuaji wa moyo kwa njia za kisasa zaidi lakini pia kupitia mtambo wetu wa Cathlab upande wa electrophysiology ambao umenunuliwa na Serikali ya awamu ya sita nitaenda kuusimamia ipasavyo ili wananchi waweze kupata huduma ya matibabu ya umeme wa moyo hapa nchini na kupunguza gharama kubwa ambayo serikali ilikuwa inatumia kupeleka wagonjwa nje ya nchi”,

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya ofisi aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji JKCI ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Prof. Mohamed Janabi aliahidi kuendelea kushirikiana na JKCI na kumuomba Mkurugenzi mpya kuiendeleza Taasisi hiyo pale alipoiacha.

Kwa upande wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Janabi alisema kikubwa atakachokwenda kukifanya ni pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa na hospitali hiyo ili huduma ziweze kuendana na hadhi ya jina la hospitali ya taifa.

“Huduma ambazo naenda kuziboresha kuanzia leo ni pamoja na huduma ile ya mtu aliyefariki katika hospitali zetu zote zilizopo eneo la muhimbili atakuwa anachukuliwa na gari la wagonjwa kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti lakini pia wagonjwa wanaotoka kitengo cha dharura kupelekwa mawodini kuanzia leo watakuwa wanabebwa na gari hilo badala ya kupelekwa kwenye vitanda”,.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya JKCI Prof. William Mahalu alisema anaamini Mkurugenzi aliyeteuliwa kuiongoza JKCI atafanya vizuri kwani amekuwa akifanya naye kazi kwa muda mrefu hivyo kumtaka kuendeleza yale yaliyoachwa na mkurugenzi aliyemaliza muda wake.

“Nawaomba wafanyakazi wamuunge mkono na kushirikiana na Mkurugenzi mteule kwa kila hali kama ambavyo walikuwa wakishirikiana na mkurugenzi aliyemaliza muda wake, ninachofurahi ni kwamba watumishi wa hapa wanamfahamu mkurugenzi mteule hivyo haitakuwa ngumu kufanya naye kazi”,.

“Ahadi zilizotolewa na Mkurugenzi mpya naamini zote zina nia ya kuboresha huduma na kung’arisha nyota ya taasisi hii, mimi kama mwenyekiti wa bodi nimezichukuwa na nitazisimamia kuhakikisha kuwa ahadi hizo zinatekelezwa”, alisema Prof. Mahalu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...