Na Said Mwishehe, Michuzi TV

RAIS Samia Suluhu Hassan amefuta mashamba makubwa 14 yenye ukubwa wa ekari 23,016 katika Halmashauri za Mvomero na Kilosa ili yagawiwe kwa wananchi jambo ambalo limeelezwa ni heshima kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro.

Akizungumza leo Oktoba 4,2022 mbele ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Shaka Hamdu Shaka wakati wa uzinduzi wa msimu wa kilimo Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa mkoa huo Fatma Mwasa amesema mashamba hayo yameanza kugawanywa kwa wananchi kwa mfumo wa Block Farming ili kuongeza ufanisi zaidi.

“Pia wakulima watapewa elimu ya kuunda AMCOS ili kurahisisha usimamizi.Aidha Serikali katika kuhakikisha wakulima wanaongeza uzalishaji imetoa ruzuku kwa mbolea za kupandia na kukuzia, mbolea ya UREA ,DAP zinauzwa kwa bei ya ruzuku ya Sh.70,000 kwa mfuko wa kilo 50.Bei bila ruzuku ingekuwa Sh.130,000.

“Mbolea ya CAN ya ruzuku ni Sh.60,000 kwa mfuko wa kilo 50 wakati bei bila ruzuku ni Sh.107,007 , wakati mbolea ya SA bei nya ruzuku ni Sh.50,000 kwa mfuko wa kilo 50 wakati bei bila ruzuku ni Sh.81,474. Uandikishaji wakulima kwenye mfumo unaendelea na tutaendelea kuwahamasisha wakulima kujitokeza kwa wingi kujisajili waweze kupata mbolea kwa bei ya ruzuku,”amesema Mwasa.

Aidha amesema Mkoa wa Morogoro kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kupitia Wizara ya Kilimo umetenga Sh.bilioni 15.2 kwa ajili ya kuendeleza miradi mitatu ya umwagiliaji ambayo ni mradi wa Rudewa –Kilosa, Idete –Mlimba na Mgongola –Mvomero.

“Uboreshaji wa miundombinu hii itawezesha wakulima kulima zaidi mara mbili kwa mwaka.Naomba utufikishe shukrani zetu za dhati kwa Rais kuendelea kutuletea miradi mikubwa ya kuboresha kilimo,”amesema.

Amefafanua leo mkoa wa Morogoro wamezindua msimu wa kilimo katika mkoa huo ikiwa ni ishara ya kuanza kwa msimu, hivyo kila mmoja atimize wajibu wake na kwamba wakulima hawana budi kuingia shambani na kuanza kuandaa mashamba yao na kuhakikisha wanafuata kanuni bora za kilimo.

Aidha amesema kauli mbiu yao ni “Agenda 10/30 vijana ni nguzo imara katika kilimo , mifugo na uvuvi , Shiriki kikamilifu kwa maendeleo ya Taifa”.Mkoa unatambua umuhimu wa vijana kushiriki katika kilimo.

Amesema ndio maana wameshiriki kuzindua shamba la vijana lenye ukubwa wa ekari 78 kwa kuanza kuwashirikisha vijana waweze kuchangia kukua kwa sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo 2030.

Mwasa amesema pamoja na uwepo wa fursa mbalimbali lakini kilimo ndicho kinachochukua nafasi kubwa na kuongeza asilimia 65 ya wakazi wa mkoa wa Morogoro hutegemea kilimo kama njia yao ya kujipatia chakula na kipato.

“Hivyo ukiboresha kilimo unakuwa umegusa asilimia 65 ya wananchi wa mkoa wetu , eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta 2,226,396 na linalolimwa ni wastani wa hekta 960,000 sawa na asilimia 40 ya eneo lote.Mazao yanayolimwa kwa wingi ni pamoja na mpunga, miwa, katani , mahindi , migomba, pamba, alizeti, ufuta , korosho, kokoa na jamii mikunde kunde na bustani za mbogamboga.

“Takribani zaidi ya miaka 10 sasa mkoa umekuwa ukizalisha chakula cha kutosha na ziada ambayo huuzwa nje ya mkoa , mfano msimu wa mwaka 2020/2021 uzalishaji wa mazao ya chakula ulikuwa ni tani 2,113,776.3 wakati mahitaji ya chakula yalikuwa tani 670,000.”

Pamoja na hayo amesema wamefanya hayo yote katika kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Samia kwa kukipa kilimo kipaumbele na hiyo imejidhihirisha kwenye bajeti ya kilimo ya mwaka 2022/2023 ambapo imefikia Sh.bilioni 900 kutoka Sh.bilioni 200.



Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa, akizungumza na wananchi katika mkutano wa uzinduzi wa msimu mpya wa kilimo katika Mkoa wa Morogo uliofanyika katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Ilonga, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.


Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa msimu mpya wa kilimo katika Mkoa wa Morogoro.


Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, akiwasikiliza wananchi alipotembelea moja ya mashamba yaliyotolewa na Rais Samia kwa vikundi vya wananchi wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro kabla ya kuzindua msimu mpya wa kilimo Mkoa wa Morogoro leo Oktoba 4,2022.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa akimkabidhi tuzo Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, baada ya kuzindua msimu mpya wa kilimo katika mkoa huo leo.


Mbunge wa Kilosa Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa msimu mpya wa kilimo Mkoa wa Morogo uliofanyika katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Ilonga, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...