KATIBU mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania – TFF Wilfred Kidau ameeleza kufurahishwa kwake na kazi inayofanywa na shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO) katika kuendeleza soka la wanawake nchini.
 
Kidau amesema hayo wakati akifunga mafunzo ya uongozi katika michezo kwa makocha wanawake 42 kutoka Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, kupitia Programu ya Mpira Fursa inayoendeshwa na KTO.  Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika jijini Dar es salaam, yameendeshwa na wataalamu kutoka Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.
 
Amesema ili kuunga mkono jitihada hizo, mapema mwaka 2023 TFF itaendesha kwa gharama zake mafunzo ya aina tatu ya soka kwa wanawake hao ikiwemo ukocha/ualimu, uamuzi (referee), na usimamizi/uongozi. Pia ametoa zawadi ya mipira miwili kwa kila mshiriki wa mafunzo hayo baada kuwapongeza kutokana na nidhamu waliyoionyesha katika kipindi chote cha mafunzo. 
 
Kwa upande wake mwakilishi wa kurugenzi ya elimu na mafunzo ya ufundi (TVET) katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi Fides Lubuva, amepongeza ushirikiano ulioonyeshwa na TFF katika kuendeleza programu hii ambayo ilianzishwa kwa ushirikiano baina ya KTO na TFF. Amewataka makocha hao kuhakikisha FDCs inakuwa na timu imara ili ziweze kushiriki michuano hadi ngazi ya taifa na kutoa wachezaji bora watakaoliwakilisha taifa katika michuano mikubwa.
 
Programu ya Mpira Fursa inalenga kukuza na kuendeleza soka la wanawake na wasichana kwa kuandaa wanasoka bora wa kike wenye kujiamini na kujithamini, na kama njia ya kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi. Programu hii inatekelezwa katika vyuo 54 vya mMaendeleo ya Wananchi kwa ufadhili wa Sida na MasterCard Foundation; na katika shule 108 za msingi kwa ufadhili wa taasisi ya Watoto ya shirikisho la soka barani Ulaya UEFA Foundation.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...