Na Pamela Mollel,Manyara

Wakazi takriban 50,000 katika kata ya Gehandu kwenye mji mdogo wa Mbulu, Mkoani Manyara, sasa wamepata zahanati mpya iliyojengwa kwa thamani ya shilingi milioni 287 katika kijiji cha Qatesh.

Zahanati hiyo mpya ya Qatesh imejengwa kupitia mradi wa ujirani mwema, katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara ambayo iko karibu na maeneo hayo.

Mbali na jengo la matibabu, mradi wa zahanati pia umejumuisha nyumba pacha kwa ajili ya makazi ya madaktari, nyumba hiyo pekee imejengwa kwa thamani shilingi milioni 52.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Sezaria Makota, Shirika la hifadhi za taifa (TANAPA) limechangia Zaidi ya shilingi Milioni 233 huku wakazi wa kijiji cha Qatesh wamechanga milioni 49 huku Halmashauri ya Mji wa Mbulu ikitoa shilingi Milioni 4.4.

“Mradi wa zahanati hasa ni wazo la wananchi na mara baada ya wao kuanza ujenzi ndipo TANAPA wakachangia katika ujenzi,” alisema Mkuu wa Wilaya katika hafla ya makabidhiano ya majengo na vifaa vya tiba.

Kutokana na mafanikio hayo, mkuu wa wilaya ya Mbulu amewasihi wananchi kuendelea kuona umuhimu wa kutunza maeneo ya uhifadhi na kuthamini utalii maana ni chanzo kikuu cha mapato nchini.

“Wakazi wa Qatesh wana sifa moja kubwa nayo ni ile ya ushirikishaji na ndio maana walikuwa wepesi kuleta wazo lao kwetu na sisi tukachangia ujenzi,” anasema Neema Mollel, ambaye ni Mkuu wa hifadhi wa ziwa Manyara.

Kwa mujibu wa Neema, Hifadhi ya Ziwa Manyara pia imejenga choo cha matundu sita kwa ajili ya Zahanati hiyo, kilichogharimu shilingi milioni 15.

“Hata hivyo kwa mwaka wa fedha 2021-2022, hifadhi pia iliomba fedha kiasi cha shilingi milioni 60 kwa ajili ya vifaa vya tiba na tayari manunuzi yamekwisha kufanyika,” aliongeza mhifadhi huyo.

Kwa upande wake Afisa Utalii Mkuu wa Kanda ya Kaskazini (TANAPA), Edmund Murashani anasema kuwa walinzi wakubwa wa maliasili nchini ni wakazi wa maeneo yanayozunguka hifadhi za taifa.

“Tanzania ina jumla ya hifadhi 22 zinazungukwa na vijiji Zaidi ya 10,000 katika wilaya Zaidi ya 70 nchini nzima,” alisema na kuongeza kuwa ushirikiano baina ya wananchi, serikali na uongozi wa hifadhi ni muhimu kwa maendeleo ya rasilimali za taifa.

Naye mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mbulu, Peter Sulle ameushukuru uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa kwa kuwawezesha wakazi wa eneo hilo kupata huduma muhimu ya afya.

Inasemekana kuwa kabla ya Zahanati kujengwa wanavijiji walikuwa wanasafiri umbali mrefu kutafuta huduma za tiba na wakati mwingine akina mama wajawazito walikuwa wanajifungulia njiani.

Mkuu wa wilaya ya Mbulu aliyevalia kitenge, Sezaria Makota akifungua Zahanati mpya katika kijiji cha Qatesh Wilayani Mbulu mradi ulidhaminiwa na Shirika la hifadhi za Taifa Tanapa kwa kushirikiana na wananchi
 
Mganga Mfawidhi Zahanati ya Qatesh Barnabas  Sassiyo akimtembeza  mkuu wa wilaya ya Mbulu katika Zahanati mpya
Mwenyekiti wa halmashauri ya Mbulu Peter Sulle
Afisa Utalii Mkuu wa kanda ya kaskazini (Tanapa)Edmund Murashani akizungumza umuhimu wa wananchi kulinda maliasili katika hifadhi zinazowazunguka
Mkuu wa hifadhi ya ziwa Manyara Neema Mollel akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Zahanati mpya ya Qatesh
Mkuu wa wilaya ya Mbulu Sezaria Makota Makota akizungumza  katika halfa ya uzinduzi wa Zahanati na kukabidhi vifaa tiba
Mkuu wa hifadhi ya ziwa Manyara Neema Mollel akimkabidhi mkuu wa wilaya ya Mbulu Sezaria Makota vifaa tiba vya Zahanati mpya ya Qatesh
 




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...