Mkurugenzi, Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo (UDSM), Salvatory Nyanto (PhD) (wa kwanza kutoka kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mdahalo wa siku mbili utakojadili masuala mbalimbali yakiwemo masuala ya uvumbuzi kwa kushirikiana kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA).

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MAHUSIANO mazuri yaliyoasisiwa mnamo mwaka 1962 kati ya mataifa ya Tanzania na Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA) yanatazamiwa kuwa na msaada mkubwa kwa Watanzania katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba Watanzania hao.

Tanzania kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamepata heshima ya kuanda mdahalo wa siku mbili ambao unahusu masuala ya Uvumbuzi ambayo ni sehemu kubwa ya majukumu ya Chuo hicho katika ufundishaji na ujifunzaji, utafiti na ubunifu na utoaji huduma kwa jamii.

Akizungumza wakati wa utambulisho wa mdahalo huo, Mkurugenzi, Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo (UDSM), Salvatory Nyanto (PhD) amesema ni faraja kwao kufanya midahalo kama hiyo ili kufikia jamii ya Watanzania kwa urahisi na kutatua changamoto zao mbalimbali kupitia utafiti, majadiliano, ufundishaji na ujifunzaji.

“Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ni Chuo kikongwe nchini Tanzania, mwaka jana (2022) kiliadhimisha miaka 60 ya ufundishaji, ujifunzaji, utafiti, ubunifu na utoaji huduma kwa jamii,” amesema Dkt. Nyanto
Dkt. Nyanto ameongeza: “Kama ilivyo kwa Shirika la JICA mwaka 2022 walitimiza miaka 60 ya utoaji huduma hapa Tanzania, ushirikiano huu unasaidia maendeleo vijijini lakini pia kusaidia kufikia malengo ya Serikali ya Tanzania kuhudumia Wananchi wake.”

Amesema mdahalo huo ni fursa tosha kwa Chuo Kikuu (UDSM) na Wanajumuiya ya Chuo hicho sanjari na Watanzania kwa ujumla kutumia nafasi hiyo kujifunza, kujadili masuala ya uvumbuzi yavyochangia maendeleo, pamoja na kujadili masuala ya ujasiriamali.

Aidha, Dkt. Nyanto amesema mdahalo huo utaangazia zaidi dira ya mwaka 2061 ya Chuo hicho Kikuu, ambayo inajikita katika kuongeza masuala ya mashirikiano ya kitaaluma, kuongeza wigo wa mataifishaji pamoja na kuongeza wigo wa ufundishaji, ujifunzaji na uvumbuzi.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu wa Shirika la JICA nchini Tanzania, Yamamura Naofumi amesema katika kuadhimisha miaka 60 ya shughuli mbalimbali za JICA nchini na pia kuadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa UDSM, JICA kwa kushirikiana na UDSM wameshariki kuandaa hafla chini ya “Programu ya JICA kwa Mafunzo ya Kijapani” iitwayo. 'Japan - Tanzania Innovation Forum' na mada kuu ya Jukwaa hilo itakuwa: Ubunifu kwa Ukuaji wa Taifa na Maendeleo Endelevu.

Amesema JICA na UDSM waliamua kuchagua mada hiyo baada ya mashauriano ya kina na wadau mbalimbali, “Jukwaa linatarajiwa kuja na majibu ya wazi kwa maswali kama vile: Je, Tanzania inapaswa kufanya nini ili kutumia kikamilifu rasilimali zilizopo katika ubunifu kwa ukuaji na maendeleo ya taifa?,” amesema Yamamura

“Je, kuna changamoto gani katika kukuza ubunifu, hasa miongoni mwa vijana nchini Tanzania?, Kwa kuzingatia uhusiano wetu wa miaka 60 iliyopita, je Japan na Tanzania zinawezaje kushirikiana zaidi kupitia Ubunifu katika siku zijazo?”

Mdahalo huo wa siku mbili utafanyika Februari 9 na 10, 2023 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Maktaba Kuu na utashirikisha Wanajopo mbalimbali wakiwemo Wataalamu mbalimbali kutoka nchi hizo mbili, Wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Wahadhiri kutoka Vyuo vikuu nchini Japan.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...