KATIKA kuendelea kutimiza majukumu ya kuimarisha usalama, ufanisi wa kiuchumi na biashara Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) limesaini makubaliano yasiyo ya kutoa taarifa (Non disclosure Agreement,) na Shirika la Posta na Mawasiliano la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia mradi wa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka Kigoma, Tanzania kwenda Kalame, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.


Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano hayo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) Eng. Peter Ulanga amesema Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka Kigoma, Tanzania hadi Kalame kupitia Ziwa Tanganyika unatarajiwa kuwa wa kilometa 150 hadi 160 na makubaliano hayo baina ya Nchi hizo mbili ni katika kushirikiana na kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa ufanisi.
" Mradi huu ni muhimu sana kwa Nchi zetu kwani utafungua njia za mawasiliano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Nchi jirani za Kenya, Uganda, Malawi, Msumbiji na nje ya Bara la Afrika... Pia mradi utaiwezesha Tanzania kufika katika nchi za Pwani ya Magharibi kupitia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo." Amesema. Aidha amelihakikishia Shirika la Posta na Mawasiliano la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwa, Tanzania ni moja kati ya Nchi mbili Afrika zenye uwezo wa kuunganisha bahari ya Hindi na Bahari ya Atlantiki kwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. " Tunayo miundombinu madhubuti ya mawasiliano na Serikali makini na wezeshi hivyo matarajio yetu kuwa mradi huu utafanikiwa kwa kiasi kikubwa." Amesema. Aidha ameishukuru Serikali kupitia Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye kwa miongozo, Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania kwa kushirikiana katika mradi huo pamoja na ujumbe wa Shirika la Posta na Mawasiliano la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuwasili Tanzania na kusaini makubaliano hayo muhimu yatakayowezesha kukamilisha mradi huo mkubwa wa kujenga miundombinu ya mawasiliano kwa maslahi ya Nchi hizo mbili. Akizungumza kwa niaba ya Postamasta mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Costastine Kasese ameishukuru TTCL kwa kushirikiana katika makubaliano hayo na ugeni huo ambao umetembelea maeneo mbalimbali yenye fursa la kibiashara. Amesema makubaliano hayo yatasaidia katika mawasiliano ya simu, intaneti pamoja na huduma za Posta na kueleza kuwa Shirika la Posta litashirikiana na DRC katika maeneo matatu muhimu ya biashara za mipaka, biashara mtandao pamoja na ubadilishanaji wa teknolojia na utoaji wa huduma za mawasiliano kwa njia ya Posta. Kwa upande wake kiongozi wa msafara huo ambaye Waziri mshauri wa Mkuu wa Wizara ya Posta na Mawasiliano na TEHAMA (DRC,) Azitemina Fundji Blaise ameeleza kuwa, Kongo na Tanzania wamekuwa na mahusiano mazuri na Balozi za nchi hizo zimekuwa zikionesha juhudi ya kuboresha mahusiano hayo. Amesema ushirikiano huo utaboresha na kunufaisha wananchi kupitia huduma za mawasiliano kupitia TTCL, Shirika la Posta na Mawasiliano la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Shirika la Posta Tanzania. Blaise amezihakikishia Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutufaika na mradi huo kiuchumi pamoja na biashara.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) Eng. Peter Ulanga akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano yasiyo ya kutoa taarifa (Non disclosure Agreement,) kati ya Shirika la Posta na Mawasiliano la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na TTCL na kueleza kuwa Tanzania ina miundombinu madhubuti na Serikali makini na wezeshi katika utekelezaji wa mradi huo, leo jijini Dar es Salaam.



Kiongozi wa msafara huo ambaye ni Waziri Mkuu mshauri wa Wizara ya Posta na Mawasiliano na TEHAMA (DRC,)Azitemina Fundji Blaise akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni marafiki wa muda mrefu na mradi huo utanufaisha Nchi hizo mbili kiuchumi na biashara, leo jijini Dar es Salaam.

Mwakilishi wa Postamasta mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Costastine Kasese akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa Shirika hilo litashirikiana na DRC katika kufanikisha mradi huo.

Zoezi la utiaji saini na kubadilishana hati za makubaliano likiendelea.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...