Emmanuel Oguda, Mahakama-Shinyanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma amewahakikishia wananchi na wadaawa katika Kanda hiyo kuwa, Mahakama itaendelea kuboresha huduma ya utoaji haki huku akiahidi kwamba katika kuboresha eneo la usikilizwaji wa mashauri kwa wakati, wadaawa sasa watapata nakala za hukumu siku ambayo hukumu zao zitasomwa mahakamani.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama mkoani Simiyu wakati alipokuwa kwenye shughuli za ukaguzi wa Mahakama robo ya kwanza mwezi Machi, 2023, Mhe. Matuma alisema kuwa, Kanda hiyo imejipanga kuhakikisha wananchi na wadaawa wanaridhishwa kwa kiwango kikubwa cha huduma wanazotoa.

“Jitihada zinazoendelea kufanywa na Mahakama ya Tanzania katika kuboresha huduma kwa wananchi kupitia mpango mkakati wa Mahakama wa miaka mitano 2020/2021 – 2024/2025, moja ya eneo muhimu katika mpango Mkakati huo ni kuhakikisha kuwa haki inatolewa kwa wakati,” alisema Jaji Matuma.

Mhe. Matuma aliongeza kuwa, awali nakala za hukumu zilikuwa zinatolewa kwa wadaawa ndani ya siku 21 toka kusomwa kwa hukumu na mienendo (proceedings) ilikuwa ikitolewa ndani ya siku 30 baada ya hukumu kutolewa.

Jaji Mfawidhi huyo alisema kwamba, hatua hiyo pia ni katika kutelekeza waraka wa Jaji Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2023 kufuatia Majaji na Mahakimu wote kuwa na vitendea kazi muhimu (kompyuta mpakato) hivyo kutokuwa na sababu ya kuendelea kutoa nakala za hukumu ndani ya siku 21. Katika mabadiliko hayo, Majaji na Mahakimu wote wanatakiwa kutoa nakala ya hukumu siku ya hukumu na nakala ya mienendo ndani ya siku 14 toka tarehe ya kutolewa uamuzi au toka siku ilipoombwa.

“Niwatake Majaji na Mahakimu wote wa Kanda ya Shinyanga kuzingatia waraka wa Jaji Mkuu ulioelekeza kutoa nakala za hukumu kwa wadaawa siku ya hukumu na mienendo itolewe ndani ya siku 14 toka tarehe ya kusoma hukumu. Naibu Wasajili, Watendaji wa Mahakama na Mahakimu Wafawidhi wote wanao wajibu wa kusimamia jambo hili na kuhakikisha linatekelezwa kama ilivyoelekezwa katika waraka wa Jaji Mkuu wa Tanzania” alisisitiza Jaji Matuma.

Wakati huohuo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Shinyanga aliwataka watumishi wote ndani ya Kanda hiyo, kuzingatia uadilifu katika kutoa haki, nidhamu kazini pamoja na kufuata kanuni za utumishi wa Umma katika kutoa haki. “Hatutamvumilia yeyote atakayekwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma hivyo kila mmoja anapaswa kujitathmini utendaji wake wa kila siku,” aliongeza Jaji Matuma.

Aidha, Jaji Matuma aliwataka Mahakimu na Watumishi wa Mahakama kusikiliza na kumaliza mashauri ndani ya muda uliowekwa ili kutoruhusu mashauri ya mlundikano ambayo kwa sasa hakuna ndani ya Kanda hiyo, huku akisisitiza kuwa, maeneo yenye mashauri mengi yatolewe taarifa ili uongozi wa Mahakama kupitia kikosi kazi maalum cha kumaliza mashauri uweze kushughulika na mashauri hayo kwa haraka na wananchi wapate haki yao kwa wakati.

Kwa upande wake Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Bi. Mavis Miti alitoa rai kwa Viongozi wa maeneo husika kuhakikisha wanawasilisha taarifa za nakala za hukumu zinazotolewa kila mwezi ili kuweza kufuatilia kwa ukaribu maagizo yaliyotolewa na Viongozi. Aidha, amewataka watumishi wote wa Mahakama kuzingatia maadili na kufanya kazi kwa weledi.

Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu MKazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga ameahidi kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Jaji Mfawidhi kuhusu nakala za hukumu kutolewa siku ya hukumu pamoja na kusimamia maadili na nidhamu kwa watumishi wa Mkoa wa Simiyu ili lengo la Mahakama la kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati litimie.

Akiongea kwa niaba ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya Maswa, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Peter Pondo aliushukuru uongozi wa Mahakama Kanda Shinyanga kwa kuendelea kuwasimamia watumishi, kuwapa mafunzo mbalimbali katika kazi zao za kila siku pamoja na kuahidi kutekeleza maelekezo yanayoendelea kutolewa na viongozi wa Mahakama Kanda.

Mhe. Matuma ameendelea na ziara yake ya ukaguzi wa Mahakama katika Mkoa wa Simiyu ambapo ametembelea Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mahakama za Wilaya Maswa, Meatu, Itilima, Busega na Bariadi.


Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma (katikati) akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Maswa (hawapo katika picha) wakati wa ziara yake ya ukaguzi. Wengine ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga (kushoto) na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Bi. Mavis Miti (kulia).
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Maswa wakimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma (hayupo katika picha) alipokuwa akizungumza na Watumishi hao wakati alipotembelea Mahakama hiyo katika ziara ya ukaguzi wa Mahakama hivi karibuni.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga (aliyesimama) akizungumza jambo wakati wa ziara ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga alipotembelea Mahakama ya Wilaya Maswa hivi karibuni.


Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Malampaka Maswa, Mhe. Peter Pondo akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya Maswa wakati wa ziara ya Jaji Mfawidhi.(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...