* TBA yaja na mfumo wa 'Smart Lock ' katika ukusanyaji kodi

WAZIRI Wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amepongeza ubunifu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) wa kuweka miundombinu ya kisasa katika nyumba za makazi ya watumishi wa Umma kwa lengo la kukusanya kodi kwa wakati na kuongeza mapato yatakayowezesha utekelezaji wa miradi mingi zaidi.

Prof. Makame ameeleza hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya ufunguzi wa nyumba za makazi kwa watumishi wa Umma katika maeneo ya Magomeni Kota na Canadian Village; Msasani Peninsula, miradi ambayo imebuniwa na kutekelezwa na TBA.

"Tatizo la wapangaji kukaa bila kulipa kodi limepata suluhisho, katika majengo haya kuna mfumo wa 'Smart Lock' au kitasa janja...Mpangaji akimaliza kodi yake hataweza kuingia ndani hadi alipe kodi, TBA imefanya vizuri simamieni hili atakayeshindwa kulipa kodi pamoja na kutunza thamani ya nyumba aondolewe ndani ya nyumba." Amesema.

Vilevile amesema katika utekelezaji wa miradi hiyo ya majengo mawili yamegharimu shilingi Bilioni 10.32 na kaya zipatazo 28 zitanufaika na miradi.

Aidha Waziri Mbarawa amesema, Serikali imeruhusu taasisi binafsi kushirikiana na TBA kujenga nyumba bora kwa ajili ya watumishi wa Umma na kupangisha kibiashara ili kupunguza uhitaji wa makazi bora uliofikia milioni 3 huku uhitaji wa nyumba za makazi ukiongezeka hadi kufikia laki mbili kwa mwaka.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daud Kondoro amesema, miradi hiyo imegharamiwa na Serikali pamoja na fedha za ndani za Wakala hiyo ambayo pia imesimamia ubunifu na usanifu wa miradi kwa kuzingatia kanuni, sheria na viwango.

Arch. Kondoro amesema, utekelezaji wa miradi hiyo umetoa fursa za ajira kwa vijana, wanawake pamoja na mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi 'Field' na wametumia changamoto ya gharama kubwa za vifaa vya ujenzi kwa kutumia kiwanda cha Wakala hiyo kuzalisha rasilimali za ujenzi zikiwemo tofali na zege.

Amesema, TBA imepokea fedha kutoka Serikalini katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

"Serikali imetoa shilingi Bilioni 5.68 katika ujenzi wa jengo hili la makazi ya watumishi wa Umma katika eneo hili la Magomeni Kota, Ujenzi wa jengo moja Canadian village Msasani Peninsula limejengwa kwa fedha za ndani za Wakala zipatazo Bilioni 4.6.... Shilingi Bilioni 4.3 zilizotolewa na Serikali zimeelekezwa katika mradi wa Ujenzi wa nyumba za makazi ya watumishi wa Umma katika eneo la Temeke Mwisho ambako ujenzi unaendelea." Amesema.

Pia Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya miundombinu Seleman Kakoso ameipongeza TBA kwa kuweka mfumo wa kulipa kodi kidigitali na kudhibiti malimbikizo ya madeni hususani kwa taasisi za Serikali ambazo hazilipi madeni kwa Wakala hiyo.

Aidha ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha kwa TBA ili waweze kutekeleza miradi mingi zaidi itakayopunguza changamoto ya makazi kwa watumishi wa Umma na watanzania kwa ujumla.

Uzinduzi huo umehusisha jengo moja la ghorofa 7 litakalibeba kaya 16 kati ya majengo matano zaidi yatakayojengwa kwa ajili ya makazi ya watumishi wa Umma Magomeni Kota na jengo moja la ghorofa Tano litakalobeba kaya 12 kati ya majengo 16 yatakayojengwa katika eneo la Canadian village, Msasani Peninsula jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa nyumba za makazi ya watumishi wa Umma Magomeni Kota na Canadian village, Masaki jijini Dar es Salaam na kutaka TBA kuendelea kukusanya kodi na kuendelea miradi mingi zaidi, Leo jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu Seleman Kakoso (mb) akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa Serikali itatoa fedha zaidi kwa Wakala hiyo ili waweze kutekeleza miradi mingi zaidi, Leo jijini Dar es Salaam.
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daud Kondoro Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa nyumba za makazi ya watumishi wa Umma Magomeni Kota na Canadian village, Masaki jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa Wakala hiyo inaendelea kutekeleza miradi mingi zaidi nchini ili kupunguza changamoto ya makazi kwa watumishi wa Umma na watanzania kwa ujumla,Leo jijini Dar es Salaam.Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...