Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema amefanya ukaguzi maalum kuhusu uendeshaji wa usimamizi wa mikataba ya maridhiano na kukiri makosa (Plea Bargain) na shughuli za utaifishaji, makabidhiano na ugawaji wa mali zilizotaifishwa.

Kupitia ripoti ya CAG ya mwaka 2021-2022 iliyosomwa mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, CAG Kichere amesema katika ukaguzi huo maalum amebaini kuwa fedha zilizotaifishwa na kuwekwa kimakosa kwenye akaunti ya makubaliano ya hiari (Plea Bargain) badala ya akaunti za utaifishaji mali zilikuwa Shilingi Bilioni 6.1.

CAG Kichere amesema fedha zilizotaifishwa na kukabidhiwa zilikuwa Ofisi ya Hazina bila kupitia akaunti maalum za utaifishaji mali zilizokadiliwa kuwa zaidi ya Shilingi Bilioni 1.

Aidha, CAG Kichere amesema ukaguzi huo maalum umebaini kuwa kutokuwa na Daftari la utunzaji wa fedha (Cash Book) zinazotokana na utaifishaji wa mali, sanjari na kushindwa kutoa Stakabadhi za mapokezi ya fedha zilizotaifishwa kuwa sehemu ya utambulizi wa mapokezi hayo.

“Mapungufu katika kusimamia mali zilizotaifishwa kumepelekea uchakavu na kuhatarisha usalama wa mali zilizotaifishwa kutoorodheshwa kwenye Daftari la kudumu la taifa la Mashtaka, pia kutokuwepo kwa uthibitisho na makabidhiano mbele ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mali zilizotaifishwa,” amesema CAG Kichere wakati akisoma Ripoti hiyo mbele ya Rais Dkt. Samia

CAG Kichere amesema kumekuwepo malalamiko ya baadhi ya waathirika wakidai kuonewa katika zoezi hilo la kukiri makosa na utaifishaji wa mali, pia CAG amesema amebaini kukosekana kwa uwazi kwenye mchakato wa majadiliano baina ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Washtakiwa. “Hapakuwa na utaratibu rasmi katika uteuzi wa timu za kuendesha majadiliano kwa upande wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,” amesema CAG.

Hata hivyo, licha ya kukiri kuwa masuala mengine yanashughulikiwa na Vyombo vya Ulinzi na Usalama, CAG amependekeza kuundwa kwa Tume huru ya Uchunguzi ukiukwaji wa maadili na matumizi mabaya ya Ofisi ya umma katika mchakato wa makubaliano na kukiri kosa na kutaifisha mali za watuhumiwa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2021/2022 kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Charles Kichere, Ikulu Jijini Dar es salaam tarehe 29 Machi, 2023.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...