* Wizara kuingilia kati kuhakikisha madeni hayo yanalipwa

KAMATI ya kudumu ya Bunge ya miundombinu imebaini uwepo wa madeni makubwa ambayo hayalipwi na wanufaika wa nyumba za makazi zikiwemo taasisi za Serikali kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) ambao ni wasimamizi na watekelezaji wa miradi hiyo hali inayokwamisha utekelezaji wa miradi mingi zaidi kwa manufaa ya watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua mradi wa Ujenzi wa nyumba za makazi kwa watumishi wa Umma zinazojengwa Temeke Mwisho jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Seleman Kakoso ameitaka Wizara ya Ujenzi kusimamia na kuhakikisha madeni hayo yanalipwa ili TBA iendelee na miradi endelevu.

"Madeni hayalipwi, Taasisi za Serikali hazilipi kodi, Wizara isimamie ulipwaji wa madeni haya ili TBA iendelee na miradi mikubwa zaidi bila kukwamishwa....mradi huu wa Temeke utabadilisha mwonekano wa mazingira haya kama ilivyo Magomeni Kota, Masaki, na mikoani tunasisitiza TBA ilipwe fedha hizo ili kazi zaidi iendelee." Amesema.

Pia ameiomba Serikali kuiendeleza kamati ya miliki ya TBA ili kuzuia wananchi kuvamia maeneo ya wazi pamoja na kuruhusu miliki ya eneo la Arusha lililoombwa na Manispaa kufanyiwa kazi mara moja na Wakala hiyo.

Aidha ameeleza kuwa TBA ina uhaba wa rasilimali watu 300 na kufanya idadi ya wafanyakazi waliopo kutotosha katika utekelezaji wa miradi ukilinganisha na idadi ya wahitaji.

Vilevile ameiagiza TBA kujiendesha kibiashara zaidi kwa kuwa wabunifu pamoja na kushirikisha na sekta binafsi katika kuiendeleza sekta hiyo zaidi.

Pia Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameipongeza TBA kwa utekelezaji wa miradi ambayo imekuwa ikisaidia watanzania wakiwemo watumishi wa Serikali na kueleza kuwa atasimamia changamoto ya madeni lukuki ambayo taasisi za Serikali zimekuwa hazilipi kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) hali inayokwamisha utendaji kazi wa Wakala hiyo.

"Watanzania tuwe na utaratibu wa kulipa kodi za pango, TBA wanafanya kazi nzuri sana husausani katika makazi ila wapangaji, taasisi za Serikali hazilipi kodi... katika mradi huu wa Temeke na Arusha tunaweka mfumo wa 'Smart Lock ' ambao mpangaji usipolipa kodi nyumba inakuwa locked hadi utakapolipa na utaratibu huu tutaupeleka katika nyumba zote za zamani ili kila mtu alipe kodi na TBA waendelee kutekeleza miradi mingi zaidi." Amesema.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daud Kondoro amesema kamati ya kudumu ya Bunge ya miundombinu imetembelea mradi huo ujenzi wa nyumba za makazi Temeke Mwisho jijini Dar es Salaam na kukagua maendeleo ya mradi huo ambao umekamilika kwa asilimia 15.

Arch. Kondoro amesema kamati imepokea na kuipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wenye jengo moja la sakafu tisa mpaka sasa.

"Tumepokea maelekezo na ushauri uliotolewa na kamati ikiwemo kushirikiana na sekta binafsi binafsi pamoja na kutekeleza miradi kwa wakati jambo ambalo kama Wakala tumekuwa tukihakikisha miradi yote inatekelezwa kwa muda uliopangwa." Amesema.

Mradi wa Temeke Mwisho unatekelezwa kwa fedha za ruzuku na gharama za ujenzi katika eneo la Temeke Mwisho na utagharimu Bilioni 19.4 ambapo hadi sasa Wakala hiyo imepokea Bilioni 4.3 na utakapokamilika utabeba Kaya 148 na inategemewa kujengewa majengo 7 zaidi yatakayobeba Kaya 1000.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo na kueleza kuwa atasimamia changamoto ya madeni lukuki ambayo taasisi za Serikali zimekuwa hazilipi kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Leo jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daud Kondoro (kushoto,) akiteta jambo na Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya miundombinu Seleman Kakoso (katika,) na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (kulia,) mara baada ya kukagua mradi huo ambapo Arch. Kondoro alivieleza vyombo vya habari kuwa, wamepokea ushauri na maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo ikiwemo kushirikiana na sekta binafsi na kutekeleza miradi kwa wakati. Leo Jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Seleman Kakoso akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua mradi wa Ujenzi wa nyumba za makazi kwa watumishi wa Umma unatekelezwa na TBA katika eneo la Temeke Mwisho na kuitaka Wizara ya Ujenzi kusimamia na kuhakikisha madeni hayo yanalipwa ili TBA iendelee na miradi endelevu. Leo Jijini Dar es Salaam.
Mradi wa Ujenzi wa nyumba za makazi kwa watumishi wa Umma unatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) ukiendelea katika eneo la Temeke Mwisho jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...