*Kazi ya Ukaguzi inafanywa na wakala waliongia mkataba
Na Chalila Kibuda
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kuanzia Mei 23, mwaka huu vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki vinavyoingizwa nchini vitatakiwa kukaguliwa kwenye nchi vinakoagizwa ili kuepusha kuingiza vifaa vilivyokwisha muda wa matumizi.

Aidha, imewataka watengenezaji na waingizaji wa vifaa hivyo, kulipa ada ya usimamizi wa taka za kielektroniki kwa kila kifaa kinachoingizwa kama gharama za usimamizi wa vifaa hivyo vinapofika mwisho wa matumizi.

Hatua hiyo ni katika kutekeleza maazimio ya mkutano wa tano wa Taasisi za Mawasiliano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACO) kudhibiti ongezeko la taka za kielektroniki.

Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha Wasambazaji wa vifaa vya kielektroniki Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, John Daffa alisema kuwa kanuni za ubora wa vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki na usimamizi wa taka za kielektroniki za mwaka 2020 zinaelekeza kuhakikisha vifaa vyote vinavyoingia nchini havijafika mwisho wa matumizi.

Pia alisema kanuni hizo zinataka kuhakikisha kuwa vifaa vyote vilivyofika mwisho wa matumizi vinapelekwa kwa watoa huduma wenye leseni za kukusanya taka , kukarabati au kuendesha mitambo ya kuchakatwa vifaa vya mawasiliano pale vinapofika mwisho wa matumizi.

Daffa alisema TCRA ina jukumu la kusajili taarifa za vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki ambavyo vimeingizwa au kutengenezwa nchini pamoja na kuweka makubaliano na watoa huduma waliopewa leseni kwa ajili ya kukusanya na kuendesha mitambo ya kuchakatwa taka za kielektroniki.

"Kuanzia Mei 23 mwaka huu maombi yote 6a kuingiza vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki yatawasilishwa kwa njia ya mtandao kupitia https://verigates.tcra-bereauveritas.co.tz ili kuwezesha uwasilishaji wa taarifa zote za vifaa vinavyoingizwa," alisema Daffa.

Alieleza kuwa baada ya maombi yao kupokelewa, uchambuzi na tathmini kuhusiana na vifaa vitakavyoingizwa pamoja na ada ya usimamizi wa taka za kielektroniki itafanyika ili kuruhusu hatua za utekelezaji.

Alifafanua kuwa uingizaji wa vifaa vya mawasiliano nchini unahitaji leseni tofauti yaani Importation License na vifaa vyote vitakavyoingizwa nchini vinatakiwa kuhakikiwa ili kutathmini ulinganifu na mwingiliano wakati wa matumizi.

Hata hivyo, alisema kuwa mtumiaji wa vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki hatahusika katika gharama hizo na kwamba hakutakuwa na ongezeko la gharama za ununuzi wa vifaa hivyo hapa nchini.

Pia alisema suala hilo ni jipya kuanza kutekelezwa nchini licha ya kuwepo kwa kampuni ambazo zilikuwa zinakusanya taka za kielektroniki bila kufuata utaratibu maalum.

Alisisitiza kuwa TCRA itashirikiana na Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa mazingira (NEMC), katika usimamizi wa taka za kielektroniki.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) John Daffa  akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na vifaa vya mawasiliano kukaguliwa kabla ya kuingia nchini , Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waagizaji wa vifaa vya Mawasiliano wakifatilia agizo kwenye mkutano, jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...