Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Anthony Mavunde ametangaza utaratibu mpya wa kuweka namba za utambulisho (Serial Number) kwa kila mche utakaokuwa unatolewa na Serikali, lengo likiwa ni kurahisisha ufuatiliaji wa miche hiyo.

Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 01 Aprili, 2023 katika shamba la Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) la Mwele Wilayani Mkinga,Tanga alipotembelea kukagua zoezi la ufunguaji wa shamba hilo pamoja na kuzindua ugawaji wa miche zaidi ya 20,000 ya chikichi kwa wakulima, miche inayozalishwa na kugawiwa bure na serikali kupitia ASA.

"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuondokana na changamoto ya mafuta ya kula nchini, na ndiyo maana tumeweka kipaumbele katika uzalishaji wa mbegu za alizeti na miche ya chikichi. Ili tuweze kuondokana na matumizi ya bilioni 474 kwa mwaka kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi, ni lazima jitihada hizi tuzisimamie na kuziendeleza.

Ili kuwa na uhakika wa ufanisi wa miche yote tunayogawa, kama Serikali tunakuja na mfumo mpya wa kuweka namba za utambulisho kwa kila mche, sambamba na kumtambua mkulima na anaenda kuupanda mche huo wapi, na huko mbeleni tutaboresha mfuu huu wa utambuzi kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya QR Code kufuatilia uzalishaji na maendeleo ya miche hiyo kwa kutumia simu ya mkononi na kutambua ina uhitaji gani ambapo tutaweza kuihudumia na kupunguza upotevu wa miche hiyo.

Serikali kupitia Ajenda 10/30 ni kuinua ukuaji wa kilimo kufikia asilimia 10 ifikapo 2030, shabaha ambayo inaenda kufikiwa kutokana na jitihada hizi za kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za kilimo pamoja na uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija.

Katika kipindi ambacho tumepata bahati kama Wizara ya Kilimo ni kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita, Viongozi wetu wote wa juu wana utashi mkubwa wa kisiasa na kutoa mkazo kwenye kilimo kwa vitendo na si maneno, ndiyo maana bajeti ya kilimo imeogezeka na kufikia bilioni 954 mwaka 2022/2023 kutoka bilioni 294 mwaka 2021/2022.

Kutokana na ongezeko hilo la bajeti ya Wizara, bajeti ya ASA imeongezeka kutoka bilioni 10.5 mwaka 2021/22 hadi kufikia bilioni 43 mwaka 2022/23.Kupitia ongezeko hili tutaendelea kufungua mashamba ya uzalishaji mbegu,tutayewekea miundombinu ya umwagiliaji na kuzungushia uzio katika mashamba yote”Alisema Mavunde

Akieleza utendaji wa Taasisi, Afisa Mtendaji Mkuu wa ASA, Dkt. Sophia Kashenge alibainisha kuwa uendelezaji wa shamba la Mwele ni wa kimkakati ambapo wanataraji kuzalisha mbegu za kuhudumia Mikoa yote ya Kanda ya Mashariki ikiwemo Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na Tanga.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Kanali Maulid Surumbu amemshukuru Mhe. Mavunde kwa ziara yake na kusisitiza kuwa uongozi wa Wilaya utaendelea kushirikiana na ASA ili kuhakikisha shamba la Mwele linafikia uzalishaji unaotarajiwa.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...