Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (kushoto) akimnyoshea kidole Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Gabriel Mayaya (kulia) wakati akimsisitizia kukamilisha ujenzi wa miradi haraka iwezekanavyo kabla ya Julai 1, 2023 wakati wa ziara yake ya kuhimiza ukamilishaji wa miradi hiyo aliyoifanya leo Juni 1, 2023 wilayani humo.



Na Dotto Mwaibale, Manyoni

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amemtaka Mhandisi na Afisa Manunuzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa wodi ya wanaume na wanawake pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti (Mochwari) katika Hospitali ya Wilaya hiyo kabla ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya kazi hiyo kurudishwa Hazina.

Serukamba ametoa agizo hilo leo (Juni 1, 2023) katika mfululizo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha wa 2022/ 2023 ambapo zimebaki siku 19 kuisha.

Maofisa waliokali kuti kavu ni Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Gabriel Mayaya ambaye alielezwa kuwa kama fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo zilizoletwa kwenye wilaya hiyo zitarudishwa Hazina kutokana na kutokamilika kwa miradi hiyo kabla ya Juni 30, mwaka huu awe na uhakika kuwa atakuwa hana kazi.

"Mhandisi hakikisha unakamilisha ujenzi wa miradi yote kwa wakati na kama fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitarudishwa Hazina bila ya kukamilisha kazi hii utakosa kazi," alisema Serukamba kwa ukali.

Kwa upande wa Afisa Manunuzi, Joseph Nswila alielezwa kuwa iwapo kesho (Ijumaa) atashindwa kupeleka mabati ya kuezekea chumba cha kuhifadhia maiti atamuweka ndani.

Serukamba alikerwa na kasi ndogo ya ukamilishaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya hiyo kutokana na uzembe unaofanywa na viongozi kwa kushidwa kusimamia na badala yake wamewachia viongozi wa vijiji,kata na kamati za ujenzi jukumu la kusimamia.

Mkuu wa Mkoa alisema serikali imeleta fedha nyingi kwenye halmashauri kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo hivyo ni lazima wakuu wa idara wagawane kuisimamia ili iweze kukamilika kabla ya Juni 30, mwaka huu.

Alisema itakuwa jambo la ajabu kama fedha hizo ambazo zimeletwa katika mkoa huu zitarudishwa Hazina kutokana na kutokamilika miradi na kwamba hali hiyo ikitokea maana yake viongozi watakuwa wamefeli na kushindwa kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassani ambaye amehangaika kuzitafuta fedha hizo.

Miongoni mwa maafisa waliopata fursa ya kutembelea na kukagua miradi hiyo ni wataalam, watendaji wa kata, tarafa, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo na viongozi wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) wilayani humo ambao ni Wales Shechambo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwembeni, Salutary Naaly na Hossen Kheri.

Miradi aliyoitembelea na kuikagua ni ujenzi wa wodi ya wanaume, wanawake na chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, kutembelea stendi ya mabasi na eneo itakapojengwa stendi mpya, ujenzi wa madarasa Shule ya Msingi Tambukareli, ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mbwasa, Ujenzi wa Bweni la Wasichana Shule ya Sekondari ya Sasajila mradi ambao umefadhiliwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya Kintinku na ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Chikuyu.



Kesho ziara hiyo itaendelea wilayani humo kwa kukagua miradi mbalimbali na kuwahimiza wahusika kuikamilisha kwa wakati.




Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akikagua ujenzi wa wodi ya wanaume na wanawake katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni.

Diwani wa Kata ya Manyoni, akichangia jambo wakati wa ukaguzi wa eneo itakapo jengwa stendi mpya ya mabasi wilayani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi ya Tambukareli.

Baadhi ya viongozi wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Wilaya ya Manyoni ambao walishiriki katika ziara hiyo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa wodi ya wanawake na wanaume katika Hospitali ya wilaya hiyo wakiwa katika picha ya pamoja.

Muonekano wa stendi ya mabasi ya sasa ya wilaya hiyo, ambayo inatakiwa kuhamishiwa katika eneo jipya kupisha malori kuhamia eneo hilo kwa ajili ya kuanzisha chanzo kipya cha mapato wilayani humo ambapo malori hayo yametakiwa kuegeshwa hapo kuanzia kesho Juni 2, 2023 huku Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akitoa wiki tatu kwa mabasi yote ya abiria kuhamia stendi mpya baada ya kujengwa kwa miundombinu ya choo na maji katika eneo hilo.

Muonekano wa madara yanayo jengwa Shule ya Msingi Tambukareli.
Muonekano wa eneo itakapo jengwa stendi mpya.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza wakati alipokuwa akikagua eneo itakapo jengwa stendi mpya.

Muonekano wa Zahanati ya Kijiji cha Mbwasa ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 95.

Muonekano wa madarasa yanayo jengwa Shule ya Msingi, Chikuyu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza wakati akikagua ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya Sasajila.

Muonekano wa bweni la wasichana linalojengwa katika Shule ya Sekondari ya Sasajila.

Muonekano wa bweni la wasichana linalojengwa Shule ya Sekondari ya Kintinku.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...