Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda (katikati) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mauzo wa Kampuni ya Tully’s inayomiliki migahawa maarufu ya Tully's nchini Japan, Bw. Daisuke Shindo (kulia) pamoja na Meneja Mkuu wa Idara ya Bidhaa za Vinywaji wa Kampuni ya Marubeni ambayo ni mbia wa Tully’s na miongoni mwa kampuni zinazosafirisha kwa wingi kahawa kutoka Tanzania kuingia nchini Japan, Bw. Masahiko Yoshimura (kushoto) wakati wa uzinduzi wa uuzaji rasmi wa kahawa ya Tanzania kwenye migahawa hiyo katika hafla iliyofanyika jijini Tokyo tarehe 9 Juni 2023

Mhe. Balozi Luvanda (wa tatu kulia) akiwa na Bw. Shindo ( wa tatu kushoto) na wadau wengine wa Japan wakati wa zoezi la uonjaji wa kahawa ya Tanzania


Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mauzo wa Kampuni ya Tully’s inayomiliki migahawa maarufu ya Tully's nchini Japan, Bw. Daisuke Shindo wakati wa uzinduzi wa uuzaji rasmi wa kahawa ya Tanzania kwenye migahawa hiyo katika hafla iliyofanyika jijini Tokyo tarehe 9 Juni 2023


Wadau mbalimbali wa Japan wakishiriki hafla ya uzinduzi wa uuzaji wa kahawa ya Tanzania kwenye migahawa ya Tully's ya nchini Japan

Mhe. Balozi Luvanda (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Bw. Shindo (wa tatu kulia) na Bw. Yoshimura (wa tatu kushoto) na Maafisa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Japan na wadau wengine wakati wa uzinduzi wa uuzaji wa kahawa ya Tanzania kwenye migahawa ya Tully's iliyopo Japan

Balozi Luvanda akiwa katika picha na Mkurugenzi Mtendaji wa Mauzo wa Kampuni ya Tully’s inayomiliki migahawa maarufu ya Tully's nchini Japan, Bw. Daisuke Shindo


Mhe. Balozi Luvanda akionesha baadhi ya kahawa za Tanzania zinazouzwa nchini Japan


Mhe. Balozi Luvanda akihojiwa na Mtangazaji kutoka Shirika la Utangazaji la Japan-NHK, Idhaa ya Kiswahili kuhusu jitihada za Ubalozi zilivyofanikisha uuzaji wa kahawa ya Tanzania kwenye migahawa maarufu ya Tully's ya nchini Japan.


Kahawa ya Tanzania kama inavyoonekana pichani

===================================================


Kampuni ya Tully’s inayomiliki migahawa maarufu ya TULLY’s imezindua rasmi uuzaji wa kahawa ya Tanzania katika migahawa yao yote 700 iliyoko nchini Japan katika hafla iliyofanyika jijini Tokyo tarehe 9 Juni 2023.

Uzinduzi huo ambao ulienda sambamba na zoezi la uonjaji wa kahawa ya Tanzania, ulishuhudiwa na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda; Mkurugenzi Mtendaji wa Mauzo wa Tully’s; Bw. Daisuke Shindo pamoja na Meneja Mkuu wa Idara ya Bidhaa za Vinywaji wa Kampuni ya Marubeni ambayo ni mbia wa Tully’s na miongoni mwa kampuni zinazosafirisha kwa wingi kahawa kutoka Tanzania kuingia nchini Japan, Bw. Masahiko Yoshimura.

Akitoa hotuba yake katika uzinduzi huo, Balozi Luvanda alizihakikishia kampuni za Japan, uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na hata uwekezaji wanapoamua kuwekeza katika kilimo au sekta nyingine za Tanzania.

Aidha, amelitaja kuwa zao la kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini ambalo linatumika kibiashara kwa kulipatia Taifa pato kubwa kwa mauzo mengi ya kigeni. Akitolea mfano wa Japan, alieleza kuwa kwa mwaka, Tanzania inauza kahawa yake Japan, kwa wastani wa asilimia 33 ya kahawa inayolimwa nchini, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu million 15 (tani 15,000) ya kahawa yote ya Tanzania inayouzwa nchini Japan.

Balozi Luvanda alieleza kuwa, soko la kahawa nchini Japan bado ni kubwa, ikilinganishwa na matumizi na uhitaji wa Japan ambapo, Japan inahitaji wastani wa kilogramu milioni 453 (tani 453,000) za kahawa kwa mwaka na kutoa rai kwa watanzania hususan, wakulima wa zao la kahawa, watayarishaji, wasafirishaji na wafanyabiashara wa zao hili kuchangamkia fursa ya soko kubwa la Japan ambalo linakua siku hadi siku.


“Napenda kutoa wito kwa watanzania wenzangu kuzingatia ubora wa viwango kwa mazao tunayolima nchini kwani nchi nyingi tunazouza bidhaa zetu hususan, hapa Japan wanazingatia sana viwango. Hivyo, ili kulikamata soko hili la Japan ipasavyo, inatupasa kwenda sambamba na mahitaji ya kidunia ikiwemo, uzalishaji kwa viwango bora” alieleza Balozi Luvanda.


Vilevile, Balozi Luvanda alieleza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuwekeza katika miradi ya muda mrefu na mifupi pamoja na maeneo ya msingi ya kutatua changamoto za kilimo kuanzia shambani hadi sokoni ili kujihakikishia uhakika wa chakula, kulisha wengine kibiashara duniani, na pia wakulima kujipatia kipato cha kutosha ili kupunguza umaskini.


“Serikali ya Tanzania kwa kasi kubwa imewekeza kwenye rasilimali fedha na watu pamoja na uhamasishaji wa sekta binafsi kuwekeza na kukifanya kilimo kuanza kutoa ajira zenye staha hususan, kwa vijana na wanawake, ikiwa ni pamoja na hatua ya kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo na kujenga msingi imara wa utekelezaji wa mipango ya kilimo yenye kutazama Tanzania ifikapo mwaka 2050”, alieleza.

Alihitimisha hotuba yake kwa kuelezea jitihada za ubalozi za kufanikisha azma ya Serikali ya Tanzania katika mageuzi ya sekta ya kilimo ya kukifanya kuwa biashara. “Ubalozi unatekeleza jukumu kubwa la kuendelea kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini ikiwemo, mazao ya kilimo kama kahawa, kwa kuzitangaza bidhaa hizo na kutafuta wawekezaji wa kuendeleza sekta mbalimbali kama vile sekta ya kilimo hususan, kilimo cha biashara kwa mazao ya kimkakati”, alihitimisha.


Kadhalika, Balozi Luvanda alihamasisha ushiriki wa wadau wa kahawa nchini katika Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa ya Mwaka 2023 (World Specialty Coffee Conference and Exhibition 2023) yatakayofanyika jijini Tokyo kuanzia tarehe 27 hadi 29 Septemba 2023, ambayo yanaratibiwa na Ubalozi kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania. Tanzania ilishiriki kikamilifu katika Maonesho hayo kwa mwaka 2023 na manufaa yake yameonekana.

Tully’s Co. Ltd., inamiliki migahawa takribani 700 nchini Japan na imejipatia umaarufu mkubwa katika biashara ya uuzaji wa kahawa za aina mbalimbali duniani. Kahawa ya Tanzania iliyozinduliwa ni kutoka Mashamba ya Kahawa ya GDM (GDM Farms) yaliyoko Mbozi mkoani Mbeya.


Kuzinduliwa kwa kahawa ya GDM nchini Japan kunapandisha zaidi uhakika wa soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo imejizolea umaarufu mkubwa kwa ubora na radha ya aina yake na kupelekea kupewa jina maarufu la kibiashara la Kilimanjaro Coffee. Jina hili hutumika nchini Japan, kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.


Tanzania inasifika Japan kwa kutoa kahawa bora aina ya Arabica (Arabica laini - full washed na Arabica ngumu - natural) inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...