Na Karama Kenyunko Michuzi TV
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amekielekeza Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuanzisha vituo vingi katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika ukaguzi wa magari.
Amesema ni jambo zuri kwa chuo hicho kuanzisha Kituo cha ukaguzi wa magari kwani idadi ya magari yaliyopo nchini ni zaidi ya milioni 2.5 huku Dar es Salaam ikiwa na nusu ya magari hayo.
Akizungumza leo Dar es Salaam baada ya kutembelea miradi mbalimbali ya chuo hicho, ametoa wito kwa taasisi za umma na binafsi kufanya ukaguzi wa magari yao Ili kupunguza matukio ya ajali za barabarani.
Amesema ni wakati wa kutumia miundombinu hiyo kukagua magari kabla ya kuanza kutumika ili yawe na ubora.
"Naelekeza mamlaka zinazosimamia vyombo vya usafiri kuhakikisha zinakaza nati kwa lengo la kunusuru maisha ya watu wasio na hatia na nguvu kazi ya taifa," amesema Kihenzile.
Katika miradi ameelekeza NIT kukamilisha miradi yote kwa muda uliopangwa sambamba na kuhakikisha thamani ya fedha.
Ameelekeza NIT waongeze hosteli nyingi ili kuchukua wanafunzi wengi na kupunguza changamoto ya wanafunzi kupanga nje ya shule ambako hakuna mazingira rafiki.
Amesema idadi ya wanafunzi wanaongezeka sasa wamefikia 15,000 na wanatarajia wanafunzi wengi zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa chuo hicho, Profesa Zakaria Mganilwa amesema kituo cha ukaguzi wa magari kilijengwa kwa ajili ya wanafunzi wao, maofisa wa polisi wanaohusika na ukaguzi na maofisa wa bima.
Amesema wanachokifanya maofisa wa bima ni kuthamanisha gari baada ya kupata ajali na kisha kuwalipa wateja wao.
"Tumekuwa tukihamasisha umma walete magari yao Ili kujua ubora wake kwani tunakagua zaidi ya mifumo 15 hasa inayoendana na usalama wa gari,''amefafanua.
Profesa Mganilwa amesema watu ambao wanauziana magari pia Wana wajibu wa kupeleka magari hayo kufanyiwa ukaguzi kabla ya kununua ili likaguliwe na watapewa taarifa ya gari husika.
"Baada ya ukaguzi tutatoa ripoti ambayo huenda mnunuzi badala ya kununua kwa Shilingi milioni nane unaweza kuambiwa gari inahitaji matengenezo ya milioni 12 hivyo ukajikuta unanunua gari kwa milioni 20," amesisitiza.
Amesisitiza kuwa wanahamasisha watanzania watumie kituo hicho kwani ukaguzi wa gari dogo huanzia Sh 60,000 huku gharama ya magari makubwa hutegemea na mahitaji na kwamba kituo hicho kitawasaidia kuwa na uhakika wa kupunguza ajali za barabarani.
Kuhusu usimamizi wa miradi, wana miradi ya ujenzi wa majengo ya kufundishia pamoja na hosteli na kwamba watahakikisha miradi hiyo inamalizika kwa muda uliopangwa na ubora unaotakiwa.
Amesema chuo kina mshauri mwelekezi pamoja na wataalamu wa ujenzi ambao wamewashikiza katika miradi hiyo na kwamba wanamsimamia mkandarasi kufanya kazi kwa ubora unaotakiwa.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akiwa kwenye chumba cha mafunzo ya uendeshaji ndege mara baada ya kutembelea Miradi mbalimbali ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) leo Septemba 29,2023 Jijini Dar es SalaamNaibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akiwa katika kituo cha kukagulia Magari (NIT) mara baada ya kutembelea Miradi mbalimbali ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) leo Septemba 29,2023 Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akimsikiliza Mhandisi mkufunzi Hamadi Makame akielezea na kumuonesha vifaa vinavyosaidia ndege kuruka mara baada ya kutembelea Miradi mbalimbali ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) leo Septemba 29,2023 Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akimsikiliza Mhandisi mkufunzi Hamadi Makame akielezea na kumuonesha vifaa vinavyosaidia ndege kuruka mara baada ya kutembelea Miradi mbalimbali ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) leo Septemba 29,2023 Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akimsikiliza Mhandisi mkufunzi Hamadi Makame akielezea na kumuonesha Piston Engine ambayo inasaidia ndege kuwaka na kuruka mara baada ya kutembelea Miradi mbalimbali ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) leo Septemba 29,2023 Jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...