Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, ( katikati) na Balozi wa Uholanzi nchini,Mh. Wiebe de Boer, katika picha ya pamoja na Maofisa wa Ubalozi huo na baadhi ya washiriki katika kongamano hilo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ( kulia) akibadilishana mawazo na Balozi wa Uholanzi nchini,Mh. Wiebe de Boer wakati wa warsha hiyo

Washiriki wa kongamano hilo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kulia) akikabidhiwa zawadi na Balozi wa Netherlands hapa nchini,Mh. Wiebe de Boer (wa pili kutoka kushoto) wakati wa Warsha hiyo, Kutoka Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Geoffrey Kirenga na Kulia ni Mkurugenzi wa Ufugaji wa Samaki wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazaeli Madalla, Warsha hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam.

UWEKEZAJI, Teknolojia, Ubunifu na Ushirikishwaji kikamilifu wa sekta binafsi kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ongezeko la gharama ya bei ya vyakula vya mifugo na kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchini.

Imeelezwa kwamba gharama za uzalishaji wa vyakula vya mifugo ndio kichocheo cha kupanda kwa bei ya mifugo hiyo sokoni kama vile samaki, ng’ombe, kuku na aina nyingine za mifugo kulinganisha na nchini jirani.

Akizungumza na washiriki wa kongamano la siku moja la umuhimu wa kuongeza ushindani katika sekta ya vyakula vya mifugo vyenye protini, iliyoandaliwa na Ubalozi wa Uholanzi hapa nchini kwa kushirikiana na Mpango wa Kukuza Kilimo Kusini Mwa Tanzania (SAGCOT) , Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alisema kwamba ni muhimu kwa kuvutia uwekezaji kwenye sekta hiyo ili kuleta mabadiliko.

“Wadau wote wanakutana leo hii hapa kujadiliana na kuja na mapendekezo namna bora ya kupunguza gharama ya bei ya vyakula vya mifugo kwa kuongeza ubunifu, uwekezaji na teknolojia ili tuweze kupambana na mabadiliko ya tabianchi, ukame, mitaji na changamoto zingine za kibinadamu,’

“Pamoja na mambo mengine ni muhimu kwa taasisi za fedha hasa mabenki hapa nchini kuanza kutoa mikopo kwa wazalishaji wa vyakula vya mifugo hapa nchini ili kuvutia wadau wengine kuingia kwenye sekta hii,”alisema Waziri Ulega.

Aliongeza kwamba ni muhimu tuwe na malisho bora yenye viwango vya ajili ya mifugo yetu ili kuweza kuifanya sekta iwe shindani ndani ya soko la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla na kuendelea kuvutia uwekezaji zaidi kutoka nje.

Waziri Ulega alisema kwamba serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi iliamua kuja na sheria ya malisho na rasilimali ya vyakula vya mifugo ili kuweza kusimamia kikamilifu sekta hii ili kuwe utaratibu rasmi unaosimamiwa na sheria.

“Nachukua nafasi kuwaelekeza Wakala wa Maabara ya Veterinari (TVLA) kuanza utaratibu wa kuwafuata wazalishaji wa vyakula vya mifugo ambao wana viwanda vya kutengeneza vyakula vya mifugo na kuwakagua na kujiridhisha kwamba wanauza vyakula vyenye ubora unaotakiwa,” aliongeza Waziri Ulega

Alisisitiza kwamba ni muhimu kwa wakala huyo wa serikali kuanza program hiyo ya kuwatembelea wazalishaji wa vyakula vya mifugo ili kuweza kuwatambua wote ambao wamesajiliwa na makampuni yao kama wazalishaji wa vyakula vya mifugo hapa nchini na kuwapa mwongozo pamoja na kuwasaidia kuweza kufikia viwango vya kimataifa vya ubora.

“Unajua gharama za vyakula vya mifugo hapa nchini zipo juu kwa mfano bei ya sato ni mara ya pili na jirani zetu wa Kenya na hii inatokana na vyakula vya mifugo bei yake kuwa juu ,” alifafanua Waziri Ulega baada ya kufungua kongamano akijibu maswali ya waandishi wa habari.

Aliongeza kwamba kwa sasa kwa takwimu zilizopo kuna makampuni 223 yaliyosajiliwa yanayotengeneza vyakula vya mifugo hapa nchini kwa njia ya kitaalamu lakini kuna wengi bado wapo kila kona na ni jukumu la Wakala wa Maabara ya Veterinari kuweza kuwatambua na kuwapa mwongozo pamoja na mambo mengine kuchukua hatua za kisheria inapobidi.

Kwa upande wake, Balozi wa Uholanzi hapa nchini, Mheshimiwa Wiebe de Boer, alisema kwamba kongamano hilo la siku moja liliwaleta pamoja watunga sera, watafiti, serikali, wadau wa sekta husika na wazalishaji wa vyakula vya mifugo kukaa pamoja na kujadiliana jinsi ya kuja na suluhisho la kupunguza gharama za vyakula vya mifugo hapa nchini.

“Kongamano hili ni muhimu kwa wadau wote katika sekta hii muhimu la vyakula vya mifugo kwa sababu gharama zinapanda siku hadi siku na ni muhimu kwa watafiti na wadau wengine kuja na njia mbadala wa kupunguza gharama hizo,” alisema Mheshimiwa Balozi de Boer

Alisema kwamba kwa kukaa pamoja wadau wote watakuja na suluhisho na mkakati wa kuwezesha sekta iwe ya ushindani wenye uhakika wa chakula bora chenye protini kwa ajili ya mifugo hapa nchini.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Mpango wa kukuza kilimo ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Geoffrey Kirenga, alisema kwamba sekta ya vyakula vya mifugo hapa nchini ni muhimu kwa kilimo na uchumi wa nchini kwa ujumla.

“kwenye sekta hii mazao na ufugaji ambayo kwa jumla inabeba maisha, kipato na ajira kwa zaidi ya 80% ya idadi ya watu hapa nchini ni muhimu kuangaliwa kwa jicho la kipekee ili iweze kutoa matokeo chanya na hizi gharama zinazokuwa kila siku zipatiwe majawabu,”

“Utajiri wa rasilimali wa mifugo kama vile ufugaji wa kuku wa biashara hapa nchini inakadiliwa kufikia 72 millioni, huku million 28.9 ng’ombe , million 16.7 mbuzi na million 5.0 kondoo alisema Kirenga.

Akiwasilisha mada ya chakula mbadala cha mifugo chenye protini , Profesa Faustine Lekule alisema kwamba moja ya protini mbadala ni kuwahamasisha wakulima kulima soya maana ina manufaa kwa chakula cha mifugo na binadamu hapa nchini.

“Soya ina manufaa na faida nyingi kama vile inarutubisha udongo, chakula cha binadamu na mifugo na inaongeza kipato na ajira na pamoja na mambo mengine ya utapiamulo na usalama wa chakula,” alisema Profesa Lekule.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...